Jamii FM

TADIO yawahasa Wanahabari kutoandika Habari za uchochezi

10 November 2020, 17:49 pm

Waandishi wa habari hususan wa redio za kijamii Tanzania wametakiwa kuandika habari za kudumisha Amani nchini na kuacha kupendelea kuandika habari za uchochezi na zenye kuleta taaruki.

Wito huo umetolewa leo na Mwezeshaji wa mafunzo ya kujenga Amani hasa baada ya Uchaguzi Denis Mpagaze yaliyoandaliwa na mtandao wa redio za kijamii nchini (TADIO),yaliyofanyika jijini Mwanza

Mpagaze amesema kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kuandika habari za kudumisha Amani nchini na kwamba taaluma yao inaweza kujenga au kuharibu kwani jamii inaviamini sana vyombo vya habari.

Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo kutoka mtandao wa Redio za kijamii nchini Cosmas Lupoja amewataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo na kuwataka waende kuyatumia katika vituo vyao ili kujenga Amani na kuwa kichecheo cha kuleta maendeleo nchini.

Nao baadhi ya waandishi wanaoshiriki mafunzo hayo Elias Maganga kutoka Pambazuko Fm ya wilaya ya Kilombero na Mwanaidi Kopakopa kutoka Redio jamii Mtwara wameushukuru mtandao wa redio za kijamii nchini TADIO kutoa mafunzo hayo kwani yamekuja wakati mzuri na yatawasaidia katika kuandaa habari na vipindi vyao.

Mafunzo hayo siku tano yameshirikisha washiriki sabini kutoka Redio thelathini na nne za bara na visiwani pamoja na chama cha waandishi wa habari Pemba.