Jamii FM

Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara yafanya tathimini

2 November 2022, 13:17 pm

Na Gregory Millanzi

Kamati ya lishe ya Halmashauri ya Wilaya Mtwara jana Novemba 1, 2022 imefanya kikao cha tathmini na Mkataba wa Lishe wa Kata na Vijiji.

Afisa lishe wa Halmashauri ya Wilaya Mtwara Bi. Magreth Tingo amewasilisha taarifa ya tathmini na mkataba wa lishe ngazi ya kata kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2022.

Aidha, Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya amewataka Watendaji wote kuimarisha mifumo ya lishe kwenye kata zao kupitia mikutano ya lishe ya kila mwezi.

Ameendelea kwa kuwasisitiza Watendaji wa kata kuwa wanapaswa kuwaelezea Wananchi makundi ya vyakula kulingana na maeneo yao, yapangwe kwenye shule za msingi na sekondari, ofisi ya Vijiji, kata, vitongoji na ofisi za Chama na kaya zote.

Pamoja na Kuhamasisha ulimaji wa mazao ya chakula na mbogamboga kwenye kata zetu. Mazao hayo ni kama kunde, maharage na mihogo, pamoja na Kutoa elimu kwenye zahanati na vituo vya kutolea huduma ya afya kuhusu umuhimu wa mbogamboga.

Kwa upande wa Katibu Tawala wa Wilaya Thomas Salala ametoa pongezi kwa kata zilizofanya vizuri katika utoaji wa Lishe kwenye kata zao na wale waliofanya vibaya wajitahidi kutoa elimu ya lishe kwenye kata zao na kuhakikisha wanakuwa na umoja na mshikamano katika kukamilisha wajibu wao.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ambaye ni Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri Adam Shemnga ametoa shukrani kwa wajumbe waliohudhuria na kuweza kufanikisha kumaliza salama kikao hicho.

Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Msijute ambacho kimehudhuriwa na baadhi ya wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wa Kata pamoja na waandishi wa habari.