Wazee kuhamasisha amani uchaguzi serikali za mitaa mkoani Mtwara
10 October 2024, 23:10 pm
Dhamira ni kuwataka wazee kukaa na vijana na kuzungumzia suala la amani na usalama wa mkoa katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa ,uchaguzi ambao umekuwa ukishuhudia heka heka za hapa na pale za vyama vya siasa.
Na Musa Mtepa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ametoa wito kwa wazee wa mkoa huo kuzungumza na vijana ili kupunguza mivutano inayoweza kujitokeza kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Akizungumza katika mkutano na wazee Leo October 10, 2024, Kanali Sawala amesisitiza umuhimu wa kutumia lugha za staha ili kuwasaidia vijana kustahimiliana na kuweka amani.
Kanali Sawala pia amewataka wazee kuhamasisha vijana kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo huku akisisitiza kuwa ni muhimu kuchagua viongozi walio na uwezo wa kuleta maendeleo kwa jamii.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Mkoa wa Mtwara, Meja Mstaafu Mohamedi Bakari Mbwana, amepongeza wito huo na kusema wapo tayari kuwasilisha ujumbe kwa vijana ili kuhakikisha wanashiriki kwa amani katika uchaguzi.
Mkutano huu umeonekana kama hatua muhimu katika kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa amani na utulivu.