Jamii FM
Jamii FM
12 December 2024, 17:43

Haya ni matokeo ya asasi za kirai ambazo zimekuwa zikihamasisha wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi ambapo hapo awali changamoto kubwa ilikuwa ni uthubutu wa mwanamke kusimama na kupigania nafasi za uongozi mbele ya wanaume.
Na Musa Mtepa
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, wanawake wameonesha mafanikio makubwa katika Kata ya Mkunwa, ambapo jumla ya nafasi 78 kati ya 150 za uongozi zimechukuliwa na wanawake ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Moja ya mafanikio hayo ni Lukia Mnyachi kutoka kijiji cha Nyengedi, ambaye amekuwa mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa Kijiji katika vijiji sita vya kata hiyo.
Akizungumza kuhusu mafanikio haya, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Mtwara (JUWAM), Mariamu Mohamed Chimbwahi, amesema kuwa jukumu la jukwaa ni kuhamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi.
Aidha amesema kuwa furaha yao ni kuona mafanikio hayo, huku akisisitiza kuwa viongozi hawa wanapaswa kutowaangusha na kuzitendea vyema nafasi hizo, ili katika awamu nyingine nafasi zilizo salio zote zichukuliwe na wanawake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT CCM Wilaya ya Mtwara, Mwajuma Nahembe, amewapongeza wananchi wa Mkunwa kwa kuwapitisha viongozi wanawake, akisema kuwa uamuzi huo una muheshimisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kuunga mkono jitihada za wanawake katika uongozi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mtwara, Zuhura Farid, pia amewapongeza wanawake wa Mkunwa kwa mafanikio hayo, akisema kuwa hayo ni mabadiliko makubwa yasiyotarajiwa na kusisitiza kuwa mafanikio haya yasihishie tu katika uchaguzi wa serikali za mitaa, bali yanapaswa kuendelea hadi kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.
Zuhura ameongeza kuwa, viongozi wa serikali za mitaa waliochaguliwa wanapaswa kushirikiana na viongozi wa chama, kuondokana na makundi, na kuwatumikia wananchi kwa kuonyesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayofanywa na Rais Samia.

Mwamko mkubwa wa wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi katika Kata ya Mkunwa na Mkoa wa Mtwara umesababishwa na elimu zinazotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na masuala ya wanawake, kama vile Shirika la Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) kupitia programu yao ya “Mwanamke Ongoza” na Jukwaa la Wanawake Mtwara (JUWAM) kupitia programu ya “Sauti Zetu”, ambazo zinaendelea kuhamasisha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi.