Jamii FM

DC Mwaipaya aongoza zoezi la usafi Makaburi ya Msafa

23 May 2026, 11:01

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdala Mwaipaya akishiriki usafi katika eneo la Makaburi Msafa yaliyopo katika kata ya Tandika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdala Mwaipaya, ameungana na wananchi kufanya usafi katika Makaburi ya Msafa na kuhimiza jamii kuendeleza usafi wa mazingira ili kuimarisha usalama na afya ya wananchi

Na Musa Mtepa

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Ndugu Abdala Mwaipaya, mapema leo Mei 23, 2026, ameungana na wananchi kufanya usafi katika eneo la Makaburi ya Msafa yaliyopo Kata ya Tandika, Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kuendelea kuweka mazingira safi na salama ili kurahisisha upatikanaji wa eneo hilo pale inapohitajika, pamoja na kulinda eneo dhidi ya wadudu hatari na wahalifu.

Sauti ya Abdala Mwaipaya, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara

Aidha, Ndugu Mwaipaya ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha usafi hauishii katika eneo la Makaburi ya Msafa pekee, bali uendelezwe pia katika maeneo mengine ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ili kudumisha hali ya usafi wa mazingira katika wilaya hiyo.

Sauti ya Abdala Mwaipaya, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa Taka ngumu na usafishaji wa Mazingira wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Angelina Soko, amesema sababu kubwa ya kufanya usafi katika eneo hilo ni kutokana na umuhimu wake pamoja na kuondoa mazingira yanayoweza kuwa maficho ya wadudu waharibifu na wahalifu.

Sauti ya Angelina Soko, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Taka Ngumu na Usafishaji Manispaa

Aidha, Angelina Soko amesema zoezi la usafi litakuwa endelevu katika maeneo mbalimbali yenye mazingira kama hayo, huku akitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanafanya usafi katika maeneo yao ili kuimarisha hali ya usafi ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Sauti ya Angelina Soko, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Taka Ngumu na usafishaji Manispaa

Naye Diwani wa Kata ya Tandika, ambaye pia ni mwenyeji wa eneo hilo, Mhe. Haroun Haroun maarufu kama “Chai Jaba”, pamoja na baadhi ya wananchi, wamepongeza hatua ya kufanyika kwa usafi katika eneo hilo na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza shughuli hiyo ili kuondoa hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na uchafu na uchakavu wa mazingira.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Tandika na Wananchi