Jamii FM
Jamii FM
11 June 2026, 13:23

Mwanamke mwenye ujauzito wa miezi tisa anayelea watoto wawili Mtwara ameomba msaada wa vifaa vya kujifungulia na mahitaji muhimu baada ya kukabiliwa na changamoto za maisha na kukimbia vitisho vya usalama
Na Musa Mtepa
Mwanamke mmoja anayejulikana kwa jina la Mwanaidi Abeid Mnunduma, mkazi wa Mkakala, mtaa wa Lweru, Kata ya Jangwani, Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, ameiomba jamii kujitokeza kumsaidia vifaa vya kujifungulia kutokana na kuwa na ujauzito wa miezi tisa huku akiwa hana uwezo wa kumudu mahitaji muhimu ya kujifungua.
Akizungumza na Jamii FM Radio Juni 10, 2026, Mwanaidi, ambaye ni mama wa watoto wawili wanaomtegemea, amesema baada ya kugundua kuwa ni mjamzito alianza kujishughulisha na ukataji na ukusanyaji wa miti kutoka katika njia za muda zilizotengenezwa na mitambo inayofanya utafiti wa mafuta na gesi katika kitalu cha Lindi/Mtwara ili kujipatia kipato.
Hata hivyo, amesema juhudi zake zilikwama baada ya mtu mmoja aliyedai kuwa mmiliki wa eneo hilo kunyang’anya tanuli lake lililokuwa tayari kwa mauzo ya mkaa, akidai kuwa alikuwa amevamia eneo hilo bila kuomba ruhusa.
Aidha, Mwanaidi amesema kufika na kuishi katika eneo hilo akiwa mjamzito kulilenga kujihifadhi baada ya aliyekuwa mume wake kumtishia na kumtolea kauli za kumdhuru yeye pamoja na watoto wake wawili aliowapata katika ndoa ya awali.
Amesema licha ya kutoa taarifa zaidi ya mara mbili katika ofisi za kijiji kuhusu vitisho hivyo, mwanaume huyo aliendelea kumtishia pamoja na watoto wake, hali iliyomlazimu kukimbia na kutafuta hifadhi eneo lingine kwa ajili ya usalama wake.
Kwa upande wake, jirani yake, Mzee Hassani Mnawate, amesema walimpokea Mwanaidi akiwa katika hali ngumu na bila msaada wowote, ndipo wananchi wa eneo hilo walipoamua kumsaidia mahitaji ya msingi yakiwemo malazi na chakula.
Hata hivyo, amesema changamoto kubwa iliyobaki ni upatikanaji wa vifaa vya kujifungulia na mahitaji mengine muhimu kwa ajili ya mama huyo na mtoto anayetarajiwa kuzaliwa.

Nao baadhi ya wanawake wa mtaa huo, wakiwemo viongozi wa Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) Kata ya Jangwani, wamesema pamoja na msaada wa awali walioutoa, bado Mwanaidi anahitaji msaada zaidi wa vifaa vya kujifungulia pamoja na chakula kwa ajili yake na watoto wake.

Mwanaidi Abeid Mnunduma amefika Mkakala, mtaa wa Lweru, Manispaa ya Mtwara Mikindani, akitokea wilayani Masasi baada ya kudai kukimbia vitisho vya kuuawa kutoka kwa aliyekuwa mume wake.
Kwa msaada zaidi au mawasiliano kuhusu hali yake, wananchi wanaweza kutumia namba za simu 0694 941 665 au 0776 742 692.
