Jamii FM
Jamii FM
2 July 2026, 12:10

TRA Mkoa wa Mtwara imekusanya Shilingi bilioni 237 mwaka 2024/2025, sawa na asilimia 156 ya lengo, huku ikiadhimisha miaka 30 ya mamlaka hiyo na kutoa Tuzo za Rais kwa walipa kodi bora
Na Musa Mtepa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mtwara imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2024/2025 baada ya kukusanya Shilingi bilioni 237 dhidi ya lengo la Shilingi bilioni 152, sawa na utekelezaji wa asilimia 156.
Taarifa hiyo imetolewa wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya TRA pamoja na hafla ya utoaji wa Tuzo za Rais kwa Walipa Kodi kwa mwaka 2024/2025 iliyofanyika katika viwanja vya Mamlaka hayo mjini Mtwara.
Akitoa taarifa ya mamlaka hiyo kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Mtwara, Daniel Katamboi, amesema mafanikio hayo yanawakilisha ukuaji wa makusanyo kwa asilimia 104 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2023/2024, ambapo mamlaka hiyo ilikusanya Shilingi bilioni 116.6.

Katamboi amesema pamoja na mafanikio hayo, mamlaka hiyo imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mwitikio mdogo wa baadhi ya wafanyabiashara katika ununuzi na matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD), wateja kutokuwa na utamaduni wa kudai risiti, pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kushusha kiwango cha mauzo yao ili kuepuka kuingia kwenye mfumo wa matumizi ya mashine hizo.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chemba ya taifa ya Biashara, viwanda na kilimo Tanzania (TNCC) Mkoa wa Mtwara, Juma Napinda amesema katika kipindi cha miaka 30 ya TRA, mamlaka hiyo imefanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ikiwemo kuanzisha mifumo iliyorahisisha ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara pamoja na kujenga mahusiano mazuri kati ya TRA na walipa kodi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, ameipongeza TRA pamoja na wadau mbalimbali kwa kufanikisha safari ya miaka 30 ya mamlaka hiyo muhimu katika uchumi wa taifa tangu ilipoanzishwa mwaka 1996.
