Jamii FM
Jamii FM
19 June 2026, 14:28

Wananchi wametakiwa kulinda mazingira na kuachana na shughuli zinazochangia uharibifu wake ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, huku Serikali na wadau wakihimizwa kuimarisha elimu na usimamizi wa rasilimali
Na Musa Mtepa
Wananchi wametakiwa kuwa walinzi wa mazingira kwa kuachana na shughuli zote zinazochangia uharibifu wa mazingira ili kuendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri maisha ya jamii kwa namna mbalimbali.
Wito huo umetolewa leo, Juni 19, 2026, na Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Diana Shilonde, wakati akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio. Majadiliano hayo yalihusu mada ya mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa, athari zake kwa maisha ya watu, uhamaji wa watu pamoja na migogoro ya rasilimali, na yaliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la TABUFO.
Diana amesema kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuwa mlinzi wa mazingira kwa kuachana na vitendo vyote vinavyohatarisha afya ya mazingira.

Akijibu swali kuhusu nafasi ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kusaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Diana amesema Serikali imeendelea kuweka sera na sheria pamoja na kusimamia utekelezaji wake. Ameeleza kuwa miongoni mwa mikakati hiyo ni Dira ya Taifa ya Maendeleo inayosisitiza matumizi sahihi ya rasilimali za asili na hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Meneja wa Programu kutoka TABUFO, Isaac Dawa, amesema jamii haina budi kulinda misitu na uoto wa asili ili kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ameongeza kuwa Serikali na wadau wanapaswa kusimamia ipasavyo kampeni mbalimbali za uhamasishaji wa uhifadhi wa mazingira katika jamii.

Naye Afisa Miradi kutoka TABUFO, Adili Laban, amesema pamoja na elimu inayotolewa kwa jamii, Serikali ina wajibu wa kuwatumia maafisa mazingira waliopo na kutumia fursa mbalimbali za programu za kimataifa zinazolenga kusaidia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Dhamira Makolo, Francis Chiwango na Moza Seifu, waliowakilisha wananchi na makundi ya watu wenye ulemavu katika kipindi hicho, wametoa wito kwa jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutunza uoto wa asili na kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.

Shirika la Tanzania Build Future Organization (TABUFO) lenye makao makuu mkoani Mtwara, linaendelea kutekeleza mradi wa Climate Peace and Security (CLIMPSE) katika wilaya za Mtwara, Tandahimba na Newala.
Mradi huo unalenga kutathmini na kuibua uelewa kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa jamii, namna yanavyochochea migogoro na mivutano kutokana na upungufu wa rasilimali, pamoja na jinsi yanavyochangia uhamaji wa watu na wanyama kutoka eneo moja kwenda jingine.