Jamii FM
Jamii FM
25 June 2026, 12:17

Wakulima wa kilimo cha kiangazi “Makoo” katika ukanda wa Ruvuma, Mtwara, wameiomba Serikali kutafuta suluhisho la kudumu dhidi ya viboko wanaovamia mashamba yao, huku wakidai changamoto hiyo kuhatarisha usalama, afya na uzalishaji wao
Na Musa Mtepa
Wakulima wa kilimo cha kiangazi maarufu kama “Makoo” kwa wakazi wa ukanda wa Ruvuma mkoani Mtwara, wameendelea kuiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la tatu kutokana na changamoto ya wanyama aina ya viboko wanaovamia na kuharibu mazao yao mashambani.
Wakizungumza na Jamii FM Radio Juni 24, 2026, wakulima hao wamesema wanalazimika kuhamia mashambani na wakati mwingine kukesha usiku kucha wakilinda mazao yao ili kukabiliana na wanyama hao, hali ambayo imeelezwa kuhatarisha afya na usalama wao.
Aidha, wakulima hao wamesema wamekuwa wakitumia tochi pamoja na kurusha mawe kama njia mojawapo ya kuwafukuza viboko hao wanapoingia mashambani nyakati za usiku.

Pia, wamebainisha kuwa licha ya kilimo hicho kuchangia kuongeza mapato ya Halmashauri, bado hawapati huduma za ugani, wakidai kuwa hawajawahi kuwaona maafisa kilimo wakitembelea maeneo hayo kwa ajili ya kuwapatia ushauri na msaada wa kitaalamu.

Akizungumza kwa njia ya simu, Afisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mkoa wa Mtwara, Kenneth Sanga, amesema changamoto hiyo inachangiwa na baadhi ya wakulima kufanya shughuli za kilimo katika maeneo ambayo ni makazi ya viboko hao.
Aidha, amewataka wakulima kuweka matuta au vizuizi kuzunguka mashamba yao ili kusaidia kuzuia viboko kuingia mashambani kutokana na maumbile na tabia za wanyama hao.