Jamii FM

Wadau waunga mkono tozo ya maendeleo ya Bandari

3 June 2026, 07:53

Wadau wa Bandari wakipata elimu juu ya tozo mpya ya maaendeleo ya Bandari katika ukumbi wa Bandari Club Mjini Mtwara

Wadau wa Bandari Mtwara na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TASACS) wamepongeza kuanzishwa kwa Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari (PID), wakisema itaboresha huduma, kupunguza muda wa mizigo bandarini na kuongeza ufanisi wa biashara

Na Gregory Millanzi

Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TASACS) pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya bandari wameipokea kwa mikono miwili Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari (PID), tozo mpya iliyoanzishwa rasmi na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kupitia Kitabu cha Ushuru wa Bandari za Bahari cha mwaka 2026.

Akizungumza Juni 2, 2026 katika Ukumbi wa Klabu ya Bandari mkoani Mtwara, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TASACS), Ephraim Mwankusye, alisema kuwa wadau wameipokea kwa moyo mkunjufu tozo hiyo kutokana na manufaa makubwa yanayotarajiwa kupatikana katika kuboresha miundombinu ya bandari na huduma za usafirishaji kwa ujumla.

Mwankusye amesema tozo hiyo itasaidia kuimarisha miundombinu ya bandari na kuongeza ufanisi katika utoaji wa mizigo, jambo litakalopunguza muda wa mizigo kukaa bandarini (dwell time) na hivyo kuharakisha shughuli za biashara.

Sauti: Ephraim Mwankusye – Mwenyekiti, TASACS

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, amesema kuwa Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari inalenga kukusanya rasilimali za kifedha zitakazowezesha ujenzi, upanuzi na maboresho ya miundombinu ya bandari ili kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Nyathi ameeleza kuwa miongoni mwa faida za moja kwa moja kwa watumiaji wa bandari ni uwekezaji katika teknolojia za kisasa, mifumo ya kidijitali na otomesheni, ambayo itarahisisha na kuharakisha usindikaji wa nyaraka pamoja na utoaji wa huduma kwa ufanisi zaidi.

Sauti: Ferdinand Nyathi – Meneja wa Bandari ya Mtwara

Baadhi ya wadau wa bandari waliohudhuria mkutano huo wameeleza kuwa wameipokea kwa mtazamo chanya tozo hiyo, wakiamini kuwa itachochea maendeleo ya Bandari ya Mtwara kwa kuvutia meli nyingi zaidi za mizigo, kuongeza ushindani na kuboresha huduma kwa wateja.

Sauti: Wadau wa Bandari Mtwara

Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari imeanzishwa chini ya Sheria ya Bandari, Sura ya 166, inayoiwezesha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kukusanya ushuru kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu na kuboresha ubora wa huduma za bandari. Tozo hiyo inatarajiwa kuanza kutumika rasmi Julai 1, 2026.