Jamii FM
Jamii FM
28 June 2026, 16:54

Katika kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mtwara imepanda zaidi ya miti 100 ya matunda na kivuli katika Shule za Msingi Majengo na Tandika, Manispaa ya Mtwara Mikindani
Na Musa Mtepa
Katika kuadhimisha miaka 30 ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ofisi ya TRA Mkoa wa Mtwara leo Juni 28, 2026 imefanya zoezi la upandaji miti katika Shule za Msingi Majengo na Tandika zilizopo Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja wa TRA Mkoa wa Mtwara, Maimuna Khatibu, amesema upandaji wa miti katika shule hizo unaonesha ushiriki wa TRA katika shughuli za kijamii pamoja na kuenzi na kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.

Aidha, amesema ushirikiano kati ya TRA, wananchi na walipa kodi ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo, ikiwemo utoaji wa elimu kwa walipa kodi, akisisitiza kuwa bila ushirikiano huo TRA haiwezi kufikia malengo yake.

Kwa upande wake, Meneja Msaidizi wa TRA Mkoa wa Mtwara, Daniel Katamboi, amesema zoezi la upandaji miti ni sehemu ya shughuli za maadhimisho ya miaka 30 ya TRA tangu kuanzishwa kwake, ambapo zaidi ya miti 100 ya matunda na kivuli imepandwa katika shule hizo mbili.

Nao walimu wakuu wa Shule za Msingi Tandika na Majengo wameishukuru TRA kwa hatua ya kupanda miti katika shule hizo, wakisema itasaidia kutoa kivuli, matunda pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia,Pia wameahidi kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ili ilete manufaa yaliyokusudiwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Gwakisa Mwasyeba, pamoja na baadhi ya washiriki wa zoezi hilo, wameipongeza TRA kwa kupanda miti ya matunda na kivuli katika shule hizo, wakieleza kuwa itachangia utunzaji wa mazingira na kutoa kivuli kwa wanafunzi na walimu.
Pia wametoa wito kwa walimu na wanafunzi kuhakikisha miti hiyo inatunzwa ipasavyo ili iweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa Shule za Msingi Tandika na Majengo wameahidi kuitunza miti hiyo kwa kuhakikisha inakua vizuri na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996. Maadhimisho hayo yanafanyika katika mikoa yote nchini, huku kilele cha maadhimisho ya kitaifa kikitarajiwa kufanyika Julai 1, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
