Jamii FM
Jamii FM
21 July 2026, 21:30

Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi amezindua laini ya umeme ya kilovoti 33 kutoka Masasi hadi Newala, mradi utakaoboreshwa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea shughuli za kiuchumi wilayani humo
Na Musa Mtepa
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, leo Julai 21, 2026, amezindua njia ya kusafirishia umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 76 kutoka Masasi hadi Newala, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa Wilaya ya Newala.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Ndejembi amesema changamoto ya upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Newala imekuwa ikiwasilishwa bungeni na wabunge kwa kipindi kirefu, hivyo uzinduzi wa mradi huo utasaidia kuondoa tatizo hilo na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa uhakika.

Aidha, Ndejembi amesema uzinduzi wa njia hiyo ni hatua ya kwanza ya uwekezaji mkubwa unaolenga kuziunganisha mikoa ya Mtwara na Lindi kwenye Gridi ya Taifa. Ameeleza kuwa ujenzi wa miundombinu ya kuiunganisha mikoa hiyo na gridi ya Taifa unaendelea.
Pamoja na hayo, Waziri Ndejembi amemwagiza Mkurugenzi wa TANESCO kuhakikisha ujenzi wa kituo cha kupokea na kusambaza umeme (Switch Station) unaanza ifikapo Agosti 15, 2026, ili kuhakikisha wananchi wa Newala Vijijini wanapata umeme wa uhakika.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mradi huo umegharimu shilingi bilioni 4.65 huku akisema kuwa mradi huo ulipangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 12 kuanzia Oktoba 2025 hadi Oktoba 2026, lakini umekamilika ndani ya miezi saba pekee.

Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Mtwara, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, Dkt. Yahaya Nawanda, ameipongeza Serikali kwa kutekeleza mradi huo, akisema changamoto ya umeme ilikuwa ikikwamisha maendeleo ya shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Newala.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Newala wamesema hapo awali walikabiliwa na changamoto kubwa ya kukatika mara kwa mara kwa umeme, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli zao za kiuchumi. Wameeleza kuwa wanatarajia mradi huo utaleta huduma ya umeme ya uhakika na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.
