Jamii FM
Jamii FM
27 August 2026, 19:53

Serikali imewataka wadau wa korosho kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji na tija ili Tanzania iwe kinara duniani, huku ikisisitiza kupunguza gharama za uzalishaji na kuhakikisha wakulima wanalipwa kwa usahihi na kwa wakati
Na Musa Mtepa
Serikali imewataka wadau wa zao la korosho nchini kuweka mikakati madhubuti itakayowezesha Tanzania kuwa nchi namba moja duniani kwa uzalishaji wa zao hilo.
Hayo yamesemwa leo, Agosti 27, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa wadau wa zao la Korosho uliofanyika katika Manispaa ya Morogoro.
Malima amesema Tanzania iliwahi kushika nafasi ya pili duniani kwa uzalishaji wa korosho, nyuma ya Msumbiji, akisisitiza kuwa ni wakati sasa kwa nchi kuweka mikakati na misingi madhubuti, huku uzalendo ukipewa kipaumbele, ili kufikia nafasi ya kwanza duniani.
Aidha,ameitaka Bodi ya Stakabadhi za Ghala, kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania, kuhakikisha wanunuzi wa korosho ghafi wanapatiwa korosho kulingana na kiwango kilichoainishwa katika hati ya mchanganuo wa mauzo huku akivitaka vyama vikuu vya ushirika kwa kushirikiana naCBT kusimamia AMCOS ili kuhakikisha zinawasilisha taarifa sahihi za wakulima, kwa lengo la kuwawezesha kulipwa fedha zao kwa usahihi na kwa wakati.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof. Peter Msoffe, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha uzalishaji wa korosho unafikia zaidi ya tani milioni moja kwa kuongeza tija katika maeneo ambayo tayari yanazalisha korosho, kabla ya kufikiria kuongeza maeneo mapya ya uzalishaji.
Prof. Msoffe amesema hatua nyingine ni kupunguza matumizi ya viuatilifu na kuhakikisha vinatumika kwa usahihi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza gharama kubwa wanazokabiliana nazo wakulima katika kuhudumia mikorosho yao.

Akitoa salamu za Bodi ya Korosho Tanzania, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Brigedia Jenerali Aloyce Mwanjile, amewataka wadau na wakulima wa korosho kuwa na mtazamo chanya kuhusu matumizi ya viuatilifu vya maji, badala ya kuamini kuwa salfa ndiyo njia bora pekee ya kukabiliana na visumbufu, hususan wakati ambapo kunatokea upungufu wa salfa nchini.
