Jamii FM
Jamii FM
27 August 2026, 20:17

TARI inaendelea na utafiti wa magonjwa na visumbufu vya korosho, ikiwemo mnyauko Fusari, huku ikitumia teknolojia ya drones na AI kuboresha udhibiti wa changamoto hizo na kuongeza uzalishaji
Na Musa Mtepa
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha tafiti za visumbufu na magonjwa yanayoathiri zao la korosho nchini, ikiwemo ugonjwa wa mnyauko unaosababishwa na vimelea vya Fusari.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya utafiti wa zao la korosho nchini leo, Agosti 27, 2026, katika mkutano wa wadau wa tasnia ya korosho, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, amesema moja ya maeneo ambayo taasisi hiyo imejikita ni kufanya tafiti kuhusu visumbufu na magonjwa yanayoathiri uzalishaji wa korosho.
Amesema kwa sasa TARI inaendelea na utafiti kuhusu ugonjwa wa mnyauko Fusari, kwa lengo la kubaini aina ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo pamoja na maeneo ambako vinapatikana.

Dkt. Bwana amesema matokeo ya tafiti hizo yatasaidia kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo na kuwezesha wataalamu kubuni njia madhubuti za kuudhibiti, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji wa korosho nchini.
Aidha, Dkt. Bwana amesema pamoja na ugonjwa wa mnyauko Fusari, kumekuwa na changamoto ya mbu wa mikorosho ambao wameendelea kuathiri zao hilo.
Amesema TARI kupitia Kituo cha Utafiti Naliendele imeanza utafiti kwa kuwakusanya na kuwafanyia uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kutafuta aina ya mitego inayoweza kutumika kuwakamata shambani, pamoja na kuchunguza uwezekano wa kutumia viumbe hai katika udhibiti wao.

Sambamba na hilo, Dkt. Thomas Bwana amesema katika eneo la uhandisi wa kilimo na matumizi ya akili mnemba (AI), TARI imeanza kutumia ndege zisizo na rubani, maarufu kama drones, katika shughuli za upuliziaji wa dawa mashambani.
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yanalenga kupunguza muda wa upuliziaji wa dawa, pamoja na kupunguza athari hasi za kiafya zinazoweza kuwapata wapuliziaji wanaotumia mashine za kawaida wakati wa kunyunyizia dawa mashambani.

Kwa upande wake, Mbunge wa Newala Vijijini, Mhe. Yahya Nawanda, amezitaka Kamati ya Kilimo, Mifugo na Mazingira (KCJE), Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) pamoja na vyama vikuu vya ushirika kukaa pamoja na kutafuta namna ya kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima wa korosho.
Nawanda amesema gharama kubwa za pembejeo zimekuwa zikisababisha wakulima kuingia katika madeni, huku kiasi cha fedha wanachokusanya kutokana na mauzo ya korosho kikitofautiana na gharama wanazotumia katika uzalishaji.
Aidha, ameshauri wadau hao kushirikiana na wakulima kufanya utafiti na kubaini aina moja ya dawa inayofanya vizuri zaidi katika kudhibiti visumbufu na magonjwa ya mikorosho, ili kupunguza matumizi ya dawa nyingi na gharama za uzalishaji.
