Jamii FM
Jamii FM
4 September 2026, 16:46

Halmashauri ya Mtwara Vijijini imevuka lengo la mapato kwa mwaka 2025/2026, ikikusanya shilingi bilioni 7.5 dhidi ya bilioni 6.7, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 12
Na Musa Mtepa
Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026, baada ya kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 7.5, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 12 ya lengo lililowekwa.
Akitoa pongezi hizo jana, Septemba 3, 2026, katika kikao cha Baraza la Madiwani, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, CPA Bahati Geuzye, Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Ufuatiliaji na Ukaguzi, Bw. Robert Misungwi, amesema halmashauri hiyo iliwekewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 6.7 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema halmashauri imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 7.5, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 12 ya lengo lililowekwa.

Aidha, Misungwi amesema pamoja na pongezi hizo, halmashauri hiyo imepewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 8.2 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, hivyo inapaswa kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdalla Mwaipaya, amewataka watendaji kata na madiwani kuhakikisha wanaweka mikakati madhubuti ya kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Mwaipaya amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni halmashauri kupeleka mashine za POS katika maeneo husika, hatua ambayo itasaidia kudhibiti upotevu wa mapato katika ngazi za vijiji na kata.

Aidha, Mwaipaya amesema iwapo kuna mtendaji au eneo ambalo halifanyi vizuri katika ukusanyaji wa mapato, Mkurugenzi wa Halmashauri anapaswa kuchukua hatua, ikiwemo kufanya mabadiliko ya watendaji, ili kuboresha ukusanyaji wa mapato katika eneo husika.