Jamii FM

Maagizo ya Mwenyekiti halmashauri Mtwara Vijijini kwa DED

4 September 2026, 14:19

Mwenyekiti wa halmashauri ya Mtwara vijijini Mhe. Hassan Salamata akitoa maagizo juu ya madiwani kupewa taarifa za miradi ya maendeleo katika kata zao kutoka kwa wakuu wa idara.( Picha na Musa Mtepa)

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Hassan Salamata, amewataka viongozi kuhakikisha madiwani wanapewa taarifa kuhusu miradi na shughuli za Serikali zinazotekelezwa katika kata zao.

Na Musa Mtepa

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Ndugu Hassan Salamata, amewataka wakuu wa Idara kupitia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha Diwani wa Kata husika anapewa taarifa kuhusu tukio au mradi wowote unaotekelezwa katika kata yake.

Salamata ameyasema hayo Septemba 3, 2026, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Halmashauri hiyo.

Amesema pia endapo kutakuwa na tukio au sherehe yoyote ya kiserikali inayofanyika katika kata, Diwani wa eneo hilo anapaswa kupewa taarifa, kwa kuwa ndiye anayekutana na changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi anaowaongoza.

Sauti ya Hassan Salamata, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini

Kauli hiyo imekuja baada ya Diwani wa Kata ya Ndumbwe, Mhe. Hamisi Ali Yasini, kutaka kufahamu utaratibu unaopaswa kufuatwa pale mwekezaji anapofika katika eneo la mradi, pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na nani anayepaswa kutoa taarifa kabla ya mwekezaji kufika katika eneo hilo na kuzungumza na wananchi.

Sauti ya Hamisi Ali Yasini, Diwani wa Kata ya Ndumbwe

Akitoa ufafanuzi kuhusu swali hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Ndugu Abeid Kafunda, amesema kuna hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa na mwekezaji kabla ya kufika kwa wananchi wa eneo husika.

Sauti ya Abeid Kafunda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini