Jamii FM
Jamii FM
4 July 2026, 17:19

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limewakamata watuhumiwa wanne wa makosa ya kimtandao wanaodaiwa kuwatapeli mawakala wa fedha kwa njia ya simu, huku likitoa tahadhari kwa mawakala dhidi ya kutoa simu zao kwa watu wasiowafahamu
Na Musa Mtepa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limefanikiwa kuwakamata watu wanne wanaotuhumiwa kujihusisha na makosa mbalimbali ya kimtandao, ikiwemo utapeli wa fedha kwa mawakala wa huduma za fedha kwa njia ya simu.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 4, 2026, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Kamishina Msaidizi wa Polisi Mwandamizi (SACP) Issa Suleimani, amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kupitia kitengo cha makosa ya kimtandao.
Kamanda Suleimani amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Ibrahimu Adam Mfinanga maarufu kama DJ Ibra (27), mkazi wa Kisesa mkoani Mwanza; Steven Elias Matiko maarufu kama Kurya Boy (29), mwendesha bodaboda na mkazi wa Mwanza; George Misabi Angima (30), fundi wa kuchomelea kutoka Mkuyuni mkoani Mwanza; pamoja na Danie Thobias Marwa (20), mkazi wa Maina mkoani Mwanza.
Amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kutumia mbinu mbalimbali za kimtandao kuwatapeli mawakala wa huduma za fedha katika maeneo tofauti nchini.
Aidha, polisi wamesema watuhumiwa hao wamekamatwa na simu 10 pamoja na laini 10 za mitandao mbalimbali ya simu ambazo hazikuwa zimesajiliwa kwa majina halisi ya watuhumiwa hao, na ambazo zinadaiwa kutumika kutekeleza uhalifu huo.
Kamanda Suleimani amesema mmoja wa wahanga wa utapeli huo katika Mkoa wa Mtwara ni afisa wa Jeshi la Polisi ambaye pia amekuwa akitoa huduma za uwakala wa fedha kwa njia ya simu mjini Mtwara.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa mawakala wa huduma za fedha kuepuka tabia ya kutoa simu zao wanazotumia kufanya miamala kwa wateja na watu wasio wafahamu ili kuepuka kutoa mwanya kwa wahalifu Kutenda vitendo vya uhalifu.
Wakizungumza mbele ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, watuhumiwa George Misabo Angima na Steven Elias Matiko wamedai kuwa tangu walipowasili mkoani Mtwara wamefanikiwa kuwatapeli baadhi ya mawakala wa huduma za kifedha na kujipatia jumla ya shilingi milioni 1.5.

Kwa upande wao, Lukia Bakari Fundi ambaye ni wakala wa huduma za kifedha katika Mtaa wa Mgomeni pamoja na Iren Frank Mchihama, mmoja wa wahanga wa utapeli huo, wamepongeza Jeshi la Polisi kwa kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao huku wakielezea namna walivyotapeliwa.
