Jamii FM
Jamii FM
15 August 2026, 16:38

Wananchi wa Kata ya Msangamkuu wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Sh milioni 252.1, kilichopunguza adha na gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Kata ya Msangamkuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea Kituo cha Afya kitakachopunguza gharama na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
Kituo hicho kilichogharimu Shilingi milioni 252.1 kwa ujenzi wa awamu ya kwanza, ambapo Shilingi milioni 2.1 ni mchango wa wananchi kupitia nguvu za jamii katika kukamilisha ujenzi wake.
Wakizungumza Agosti 12, 2026 baada ya kutembelewa na Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye pia ni Waziri mlezi wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Judith Kapinga, wananchi wamesema hapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kwa gharama kubwa kupata huduma za afya, lakini sasa kituo hicho kimeleta unafuu mkubwa.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho mbele ya Waziri Kapinga, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Msangamkuu, Alfan Juma Issa, amesema kituo tayari kimeanza kutoa huduma muhimu ikiwemo huduma za wagonjwa wa nje (OPD), afya ya mama na mtoto, maabara pamoja na huduma za kujifungua.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Msangamkuu, Mohamed Sinani, ameishukuru Serikali kwa kukamilisha mradi huo na kuomba Serikali kuendelea kuwekeza katika kilimo cha mwani, ambacho ni chanzo muhimu cha kipato kwa wanawake wanaoishi katika vijiji vya mwambao wa Bahari ya Hindi wilayani Mtwara.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Mwalimu Saidi Nyengedi, amewataka wananchi kuitunza miundombinu ya kituo hicho na kuwasisitiza watumishi wa afya kutoa huduma kwa haki, weledi na utu kwa wagonjwa wote.

Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi na kukagua mradi huo, Waziri Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kutekeleza kipaumbele cha kuboresha huduma za afya kwa kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma nchini, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais kwa wananchi.
