Jamii FM
Jamii FM
16 May 2026, 12:12

Jamii Mkoa wa Mtwara imetakiwa kuwekeza zaidi katika malezi ya watoto kwa kuwajengea maadili mema na ushiriki wa wazazi wote, huku wadau wakisisitiza kuboresha vituo vya malezi na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu ukuaji timilifu wa mtoto
Na Musa Mtepa
Jamii imetakiwa kuwekeza katika malezi ya mtoto badala ya kuwekeza pekee katika utoaji wa huduma, ili kumlea katika maadili na maelekezo sahihi yatakayomuwezesha kutambua mema na mabaya katika jamii.
Wito huo umetolewa Mei 15, 2026 na Bi. Teresia Ngonyani, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mtwara, katika kikao cha nusu mwaka cha kutathmini utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJM-MMAM).
Kikao hicho kimewakutanisha wadau na waratibu mbalimbali, wakiwemo waratibu wa afya ya baba, mama na mtoto, maafisa ustawi na maendeleo ya jamii, maafisa lishe pamoja na maafisa elimu ya msingi na awali kutoka halmashauri tisa za Mkoa wa Mtwara.
Bi. Teresia Ngonyani amesema jamii inapaswa kuwekeza zaidi katika malezi ya mtoto kwa kumpa maelekezo sahihi kuhusu mambo mema na mabaya, huku baba na mama wakishiriki kwa pamoja katika jukumu hilo.

Aidha, Bi. Teresia Ngonyani amesema kuwa katika utekelezaji wa PJM-MMAM bado kuna changamoto ya uelewa mdogo wa jamii kuhusu malezi na ukuaji timilifu wa mtoto.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Abilah Mfinanga ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa anayeshughulikia mipango na uratibu, amezielekeza halmashauri zote mkoani Mtwara kuhakikisha Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto inapewa kipaumbele katika bajeti zao.
Abilah Mfinanga amesema licha ya changamoto zilizopo katika utekelezaji wa programu hiyo, bado kuna umuhimu wa kuongeza juhudi katika kuboresha upatikanaji wa vituo vya malezi na makuzi ya awali ili kuhakikisha huduma zinawafikia watoto wengi zaidi, hususan wa maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la FAWOPA Tanzania, Komba Baltazar, amesema wao asasi za kiraia wamekuwa wakitekeleza programu hiyo kupitia mradi wa vituo salama vya malezi ya awali kwa watoto huku akitoa wito kwa jamii kumiliki na kusimamia vituo vya kulelea watoto ili waweze kulelewa katika misingi bora ya maadili, kiimani na mazingira yanayowazunguka.
