Jamii FM

TAKUKURU Mtwara yafanikisha malipo ya zaidi ya  milioni 87.3 kwa wananchi

20 May 2026, 15:48

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Mwanakombo Rajabu akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya utendaji kazi katika kipindi cha mwezi January hadi March 2026(Picha na Razack Luambano)

TAKUKURU Mkoa wa Mtwara imewezesha kurejeshwa kwa zaidi ya shilingi milioni 87 kupitia miradi ya kuzuia rushwa, uchambuzi wa mifumo na ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma kati ya Januari hadi Machi 2026

Na Musa Mtepa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara, katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026, imefanikiwa kuwezesha zaidi ya shilingi milioni 87.3 kwa mamlaka za Serikali na wananchi kupitia shughuli mbalimbali za kuzuia rushwa pamoja na uchambuzi wa mifumo ya kiutendaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 20, 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Mwanakombo Rajabu, amesema kuwa kati ya fedha hizo, TAKUKURU imewezesha shilingi milioni 25 za Mfuko wa Elimu wa Wilaya ya Tandahimba.

Fedha hizo zilikuwa zimelipwa kwa mzabuni wa vifaa vya ujenzi wa mradi wa matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Msingi Mikuyu.

Hata hivyo, baada ya kupokea malipo hayo, mzabuni huyo alitoweka kusikojulikana hadi pale TAKUKURU ilipofanya ufuatiliaji na kubaini kuwa fedha hizo zilikuwa zimepokelewa. Baada ya hatua hiyo, mzabuni alirejea eneo la mradi na kuukamilisha ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Sauti ya Mwanakombo Rajabu Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara

Aidha, TAKUKURU imewezesha pia katika miradi mingine katika Mkoa wa Mtwara, Miradi hiyo ni pamoja na kurejeshwa kwa shilingi milioni 4.2 kwa ajili ya mradi wa madirisha katika Shule ya Sekondari Michiga iliyopo katika wilaya ya Nanyumbu, pamoja na shilingi milioni 34.4 za malipo kwa wakulima 35 wa zao la korosho kwa msimu wa 2025/2026.

Malipo hayo yalitoka katika AMCOS za Namahonga, Langana, Kuchele, Chimbuko, Madaba na Bahari zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.

Sauti ya Mwanakombo Rajabu Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara

Katika hatua nyingine, TAKUKURU imeendelea kufuatilia matumizi sahihi ya rasilimali za umma ambapo ilikagua jumla ya miradi 32 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7.8 katika sekta za barabara, afya, ujenzi, elimu, maendeleo ya miji na utawala.

Kupitia ufuatiliaji huo, taasisi hiyo imebaini kasoro mbalimbali zikiwemo ujenzi usiozingatia michoro iliyosanifiwa, matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora pamoja na wizi wa vifaa vya ujenzi.

Sauti ya Mwanakombo Rajabu Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara