Jamii FM
Jamii FM
18 June 2026, 12:22

Wananchi wa Lwelu wameiomba Halmashauri ya Mtwara Mikindani kuboresha barabara za vumbi kutokana na ubovu unaowakwamisha kupata huduma muhimu na kusafirisha mazao yao kwa urahisi
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Mtaa wa Lwelu, Kata ya Jangwani Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mkoani Mtwara ,wameiomba Halmashauri kuangalia kwa jicho la tatu hali ya barabara za vumbi zinazounganisha maeneo mbalimbali ya mtaa huo kutokana na ubovu wake.
Wakizungumza na Jamii FM Radio Juni 16, 2026, wananchi hao wamesema ubovu wa barabara hizo umekuwa kero kubwa, hususan wakati wa dharura za kuwapeleka wajawazito hospitalini kwa ajili ya kujifungua, kusafirisha mazao yao pamoja na kufuata huduma nyingine muhimu mjini.
Aidha, wameeleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakipewa ahadi za ujenzi na ukarabati wa barabara hizo bila kuona utekelezaji wake, hali ambayo imeendelea kuwa changamoto kubwa kwao. Wamesema pia gharama za usafiri kwa kutumia bodaboda zimeongezeka kutokana na ubovu wa miundombinu hiyo.
Akizungumzia kero hiyo, Diwani wa Kata ya Jangwani ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mhe. Saidi Mohamed Zaid, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo.
Amesema Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) tayari imefahamu tatizo hilo na inaendelea na jitihada za kutafuta ufumbuzi wa haraka ili kuboresha barabara hizo na kupunguza adha kwa wananchi.
Mhe. Zaid amewataka wananchi kuendelea kuwa na subira wakati taratibu za upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa maboresho hayo zikiendelea.
