Jamii FM
Jamii FM
13 August 2026, 19:05

Waziri Judith Kapinga amewataka watumishi wanaosimamia biashara kutoa mrejesho wa haraka kwa wafanyabiashara, huku Jumuia ya Wafanyabiashara Mtwara ikiwasilisha changamoto za kodi, tozo na ombi la viwanda pamoja na kivuko cha Kilambo
Na Musa Mtepa
Serikali imesema watumishi na taasisi zilizopewa jukumu la kusimamia maendeleo ya biashara wanapaswa kubadilika kwa kutoa mrejesho wa haraka kuhusu changamoto zinazowasilishwa na wafanyabiashara, ili kuendana na kasi ya utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 12, 2026 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, wakati wa kikao kilichowakutanisha wajasiriamali wadogo na wafanyabiashara wa Mkoa wa Mtwara kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), tawi la Mtwara.
Mhe. Kapinga amesema mtu anayeelewa na kutafakari maono ya Rais hawezi kupuuza umuhimu wa kuwasikiliza wafanyabiashara, kwani wao ndio nguzo kuu ya sekta binafsi na uchumi wa taifa.

Aidha, Waziri Kapinga amesema zama za kuongoza kwa misingi ya uthibiti pekee zimepitwa na wakati, akieleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mitaji ya sekta binafsi inahitaji mazingira ya uwezeshaji badala ya vikwazo, ili wafanyabiashara waweze kukuza biashara zao na kuongeza ajira.
Kwa upande wake, Makamu mwenyekiti kwa niaba ya katibu wa Jumuia ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mtwara Ndug, Selemani Kadege ,amesema hali ya biashara mkoani Mtwara ni ya wastani na inaendelea kuvutia uwekezaji kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wafanyabiashara na viongozi wa Serikali, hususan Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hata hivyo, Kadege amesema pamoja na mafanikio hayo, bado wafanyabiashara wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo utitiri wa kodi na tozo unaosababisha usumbufu katika masoko na maeneo ya biashara.
Sambamba na hilo, amemuomba Waziri wa Viwanda na Biashara kufikisha kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ombi la kujengwa kwa viwanda vya mbolea na viatilifu vya mazao mkoani Mtwara, pamoja na kurejeshwa kwa kivuko cha Kilambo kinachounganisha Tanzania na Msumbiji, akisema huduma hiyo itaimarisha biashara ya mipakani na kukuza uchumi wa Mkoa wa Mtwara.
