Jamii FM

TARI Naliendele yaimarisha utafiti kwa Teknolojia Mpya

14 August 2026, 16:30

Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu kwa niaba ya mkuu wa mkoa akizindua vifaa vipya vya utafiti katika kituo cha utafiti wa kilimo TARI-Naliendele Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

TARI Naliendele imezindua vifaa vya kisasa vya utafiti na miundombinu vitakavyoongeza ufanisi, kuharakisha tafiti na kuinua tija katika uzalishaji na kuongeza thamani ya zao la korosho nchini

Na Musa Mtepa

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Naliendele, imezindua vifaa vya kisasa vya utafiti na miundombinu vitakavyosaidia kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa kazi na kuinua tija katika uzalishaji wa korosho nchini.

Uzinduzi huo umefanyika Agosti 13, 2026 katika viwanja vya TARI Naliendele, vilivyopo Kata ya Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Christopher Magala, amewataka watafiti na watumiaji wa vifaa hivyo kuvitunza na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili vizalishe matokeo yenye manufaa kwa taasisi na wananchi.

SAUTI: CHRISTOPHER MAGALA – MKUU WA WILAYA YA NANYUMBU

Magala amesema ni muhimu kwa TARI kuhakikisha tafiti zinazofanywa kwa kutumia teknolojia mpya zinatoa suluhisho zinazoweza kutumiwa na wakulima, viwanda na sekta binafsi ili kuongeza tija na thamani ya zao la korosho.

Amebainisha kuwa maeneo ya kipaumbele ni pamoja na uzalishaji wa mbegu bora, kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu, pamoja na kuongeza thamani ya korosho kupitia usindikaji.

SAUTI: CHRISTOPHER MAGALA – MKUU WA WILAYA YA NANYUMBU

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Thomas Bwana, amesema mafanikio ya utafiti yanategemea uwepo wa watafiti wenye uwezo, usafiri wa uhakika na vifaa bora vya kisasa, ndiyo maana taasisi imeamua kuwekeza katika teknolojia hiyo.

SAUTI: THOMAS BWANA – MKURUGENZI MKUU WA TARI

Akizungumzia matumizi ya ndege nyuki (droni), Mkurugenzi wa TARI Naliendele, Dkt. Geraldina Mzena, amesema teknolojia hiyo ina uwezo wa kutambua ukubwa na urefu wa miti ya korosho na kurahisisha unyunyiziaji wa viuatilifu kwa usahihi, huku ikiwa salama kwa afya ya binadamu.

SAUTI: DKT. GERALDINA MZENA – MKURUGENZI WA TARI NALIENDELE

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Frances Alfredi, pamoja na Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmed Katani, wamekipongeza Kituo cha TARI Naliendele kwa mchango wake katika maendeleo ya zao la korosho na kuomba tozo ya utafiti iendelee kuimarishwa ili kuboresha tasnia ya korosho nchini.

SAUTI: FRANCES ALFREDI NA KATANI AHMED KATANI

Vifaa vilivyozinduliwa ni pamoja na Gari mbili,pikipiki 20 kwa ajili maafisa utafiti,Ndege Nyuki (Dron)itakayotumika katika umwagiliaji wa viuatilifu kwenye Mikorosho,Maabara mpya ya kisasa pamoja na Maboresho ya ofisi kwa ajili ya maafisa utafiti wa kituo hicho.