Jamii FM

CRDB Nanauka CUP 2026 yazinduliwa rasmi Mtwara

14 June 2026, 14:31

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akiwa naWaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana na mwanzilishi wa mashindano hayo, Dkt. Joel Nanauka wakionesha zawadi ya mashindano hayo(Picha na Musa Mtepa)

Mtwara Festival Nanauka Cup 2026 imezinduliwa rasmi Mtwara, huku viongozi wakisisitiza umuhimu wa michezo katika kuibua vipaji vya vijana. Mashindano hayo yanatarajiwa kutoa fursa kwa TFF kutambua na kukuza wachezaji watakaolitumikia taifa siku zijazo

Na Musa Mtepa

Msimu wa burudani wa Mtwara Festival Nanauka Cup 2026 umezinduliwa rasmi leo, Juni 13, 2026, katika viwanja vya Nangwanda Sijaona, Manispaa ya Mtwara.

Akizindua mashindano hayo, mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amempongeza mwanzilishi wa mashindano hayo kwa ubunifu na juhudi za kuibua vipaji vya vijana kupitia michezo.

Aidha, Mheshimiwa Kikwete amesema kuwa mbali na kupewa heshima ya kuzindua mashindano hayo, amejifunza namna maandalizi yake yalivyofanyika, huku akitoa wito kwa kocha wa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 17 (U-17) kutenga muda wa kutembelea Mtwara ili kushuhudia na kutambua vipaji vilivyopo mkoani humo.

Sauti ya Ridhiwani Kikwete waziri wa utumishi wa umma

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana na mwanzilishi wa mashindano hayo, Dkt. Joel Nanauka, amesema ana matumaini makubwa kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litapata vipaji vipya kutoka Mtwara kupitia mashindano hayo.

Sauti ya Dkt Joel Nanauka Mbunge wa Jimbo la Mtwara

Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),Athumani Nyamlani , amempongeza Dkt. Nanauka kwa kuanzisha mashindano hayo, akisema yatasaidia kugundua vipaji vitakavyoiwezesha Tanzania kupata wachezaji bora kwa ajili ya timu za taifa. Aidha, ameahidi kuwa katika mashindano yajayo TFF italeta wataalamu zaidi watakaosaidia kung’amua vipaji vya michezo mkoani Mtwara.

Sauti ya Athumani Nyamlani Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Akitoa taarifa kuhusu mashindano hayo, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Mohamedi Tilika, amesema kuwa awamu ya kwanza ya Mtwara Festival itahusisha matukio mbalimbali ya michezo ikiwemo mpira wa miguu, riadha, netiboli pamoja na ligi za bao na drafti.

Sauti ya Mohamedi Tilika

Pia, Tilika amesema kuwa michezo ya Nanauka Cup 2026 itafanyika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona kwa ajili ya mchezo wa ufunguzi na fainali, pamoja na viwanja vya Shule ya Msingi Chikongola, TARI Naliendele na uwanja wa Titanic uliopo Mikindani. Amesema mshindi wa kwanza wa mashindano hayo anatarajiwa kujinyakulia kitita cha shilingi milioni tatu za Kitanzania.

Sauti ya Mohamedi Tilika