Jamii FM
Jamii FM
28 April 2026, 11:19

Bodi ya Korosho Tanzania yaanza kusambaza zaidi ya tani 50,000 za pembejeo, ikiwemo salfa na viuatilifu, huku wakulima wakihimizwa kutumia kwa usahihi kuongeza uzalishaji wa korosho nchini.
Na Musa Mtepa
Zoezi la usambazaji wa pembejeo za zao la korosho limeanza rasmi kwa msimu wa kilimo wa 2026/2027, huku matarajio yakionyesha zaidi ya tani 50,000 za pembejeo kusambazwa katika mikoa yote inayolima korosho nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Meneja wa Mipango ya Kilimo, Juma Yusufu, amesema bodi imejipanga kusambaza tani 30,000 za salfa ya unga pamoja na lita milioni 1.5 za viuatilifu vya maji na kuongeza kuwa mfumo wa kidigitali utaendelea kutumika katika kurahisisha usambazaji na ugawaji wa pembejeo hizo kwa wakulima.

Aidha, Juma Yusufu amesema CBT kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imejipanga kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi na salama ya pembejeo hizo, hatua inayolenga kuongeza tija na uzalishaji wa korosho nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Ushirika wa mradi wa pamoja wa vyama vikuu vya korosho nchini (KCJE), Mabruki Mpangula, amesema tayari wana tani 16,000 za salfa zilizobaki kutoka msimu uliopita. Ameongeza kuwa wameingia mkataba na wazabuni kwa ajili ya kuagiza tani 35,000 zaidi, na hivyo kufanya jumla ya matarajio kufikia tani 51,000 za salfa kwa msimu mzima wa 2026/2027.
Naye Afisa Kilimo kutoka Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU, Salumu Faki, amewataka wakulima kuwa tayari kupokea pembejeo hizo na kuanza matumizi ya viuatilifu vya maji kwa wakati ili kudhibiti wadudu waharibifu wa mikorosho.
