Jamii FM

Jamii Mtwara yaaswa kuepuka matumizi holela ya Dawa

20 June 2026, 12:07

Maafisa wa Afya kutoka Hospitali ya Kanda ya Kusini wakitoa Elimu ya matumizi sahihi ya Dawa

Wataalamu wa afya Mtwara wameitaka jamii kuacha kutumia dawa bila vipimo na ushauri wa daktari, wakionya kuwa matumizi yasiyo sahihi yanaweza kusababisha madhara na usugu wa vimelea dhidi ya dawa

Na Musa Mtepa

Jamii imetakiwa kuachana na tabia ya kutumia dawa bila kufanyiwa vipimo na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

Rai hiyo imetolewa Juni 15, 2026, na Mfamasia wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara, Philemon Mwakikali, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio, ikiwa ni sehemu ya utoaji wa elimu kwa umma katika maadhimisho ya wiki ya Famasia.

Philemon amesema kuwa dalili za baadhi ya magonjwa zinaweza kufanana, hivyo si salama kwa mtu kujinunulia dawa bila kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa mgonjwa kumuona daktari ili afanyiwe vipimo na kupewa dawa sahihi kulingana na tatizo la afya lililobainika.

Sauti ya Philemon Mwakikali, Mfamasia

Aidha, amebainisha kuwa matumizi yasiyo sahihi ya dawa yanaweza kusababisha madhara mbalimbali, ikiwemo kuongezeka kwa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, hali inayoweza kufanya tiba kushindwa kufanya kazi ipasavyo.

Sauti ya Philemon Mwakikali, Mfamasia

Kwa upande wake, Mteknolojia Dawa katika hospitali hiyo, Husein Mwinyi, ameihimiza jamii kuhakikisha inamaliza dozi zote walizoandikiwa na daktari, kuepuka tabia ya kuchangiana dawa, pamoja na kuacha kutumia sindano bila sababu za msingi za kitabibu.

Amesema vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha afya ya mgonjwa na kuongeza hatari ya madhara yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

Sauti ya Husein Mwinyi, Mkuu wa Teknolojia ya Dawa

Hata hivyo, Husein ameishauri jamii kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara katika vituo vya kutolea huduma za afya, hata pale mtu anapokuwa hajisikii kuumwa, ili kubaini mapema changamoto za kiafya na kupata tiba stahiki

Sauti ya Husein Mwinyi, Mkuu wa Teknolojia ya Dawa