Jamii FM

Tume ya Haki za Binadamu yatoa mafunzo kwa wavuvi wadogo Mtwara

16 June 2026, 10:32

Afisa wa Tume ya Haki za Binadamu na utawala Bora akitoa mafunzo kwa wavuvi na watumiaji wa rasilimali Bahari wa kijiji cha Msangamkuu halmashauri ya Mtwara Vijijini (Picha na Musa Mtepa)

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa mafunzo kwa wavuvi wadogo Msangamkuu kuhusu haki za binadamu, matumizi sahihi ya rasilimali za bahari na namna ya kushughulikia matukio ya uvunjifu wa haki ili kupunguza migogoro

Na Musa Mtepa

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa mafunzo kuhusu haki za binadamu kwa wavuvi wadogo wa Kijiji cha Msangamkuu kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu haki hizo na namna ya kuzifikia pale zinapovunjwa.

Akizungumza Juni 15, 2026, wakati wa mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Patience Ntwina, amesema wamebaini kuwa utekelezaji na usimamizi wa matumizi ya rasilimali za bahari umekuwa na changamoto mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha kila mtu ananufaika na rasilimali hizo bila kuingiliana au kuathiriana kati ya wavuvi na wakulima wa mwani.

Sauti ya Patience Ntwina, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu

Aidha, Ntwina amesema kuwa si Msangamkuu pekee itakayonufaika na mafunzo hayo, bali pia maeneo mengine ya ukanda wa pwani mkoani Mtwara yatapatiwa elimu hiyo. Amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mafunzo hayo ili kila mmoja aweze kunufaika na rasilimali za bahari bila kuvunja haki za binadamu za wengine.

Sauti ya Patience Ntwina, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu
Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Patience Ntwina,akizungumzia dhamira na lengo la mafunzo kwa wavuvi wadogo katika kijiji cha Msangamkuu

Kwa upande wake, Katibu wa BMU wa Kijiji cha Sinde, Faruck Hilari, amesema kuwa moja ya sababu zinazochangia migogoro kati ya wadau wa matumizi ya rasilimali za bahari ni ukosefu wa uelewa wa kutosha katika usimamizi wa sheria na kanuni. Amesema mafunzo hayo, yaliyowakutanisha wadau mbalimbali, yatasaidia kupunguza migogoro hiyo, huku akiiomba Serikali na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali za bahari.

Sauti ya Faruck Hilari, Katibu wa BMU Kijiji cha Sinde

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata itawasaidia kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika shughuli za matumizi ya rasilimali za bahari, pamoja na kuwajengea uwezo wa kutambua na kuchukua hatua wanapokumbana na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu.

Sauti za washiriki wa mafunzo