Jamii FM
Jamii FM
10 August 2026, 23:57

Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga amezitaka CAMARTEC na WRRB kuwawezesha wananchi kupata mashine za kuchakata korosho, kuongeza thamani ya zao hilo, ajira na kipato.
Na Musa Mtepa
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amezitaka kituo cha zana na Teknolojia za Kilimo na Maendeleo ya Vijijini( CAMARTEC) na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) kuweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia wananchi mmoja mmoja na vikundi kupata mashine zitakazowawezesha kuongeza thamani ya zao la korosho.
Waziri Kapinga ametoa agizo hilo leo, Agosti 10, 2026, wakati wa uzinduzi wa Kiwanda Darasa cha CAMARTEC kilichojengwa katika Kijiji cha Mandiwa, Kata ya Chikukwe, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Amesema licha ya serikali kuweka kiwanda hicho katika eneo hilo, mahitaji ya wananchi bado ni makubwa, hivyo taasisi hizo zinapaswa kuweka utaratibu utakaowawezesha wananchi mmoja mmoja na vikundi kupata mashine za kuchakata korosho na bidhaa zake.

Aidha, Waziri Kapinga amewahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwa sehemu ya juhudi za kuleta maendeleo kwa wananchi, ikisisitiza kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi katika maeneo mbalimbali zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta tija kwa jamii.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa KIDAKUKU, Mhandisi Godfrey Mwinama, amesema mradi huo umetumia shilingi milioni 600, fedha ambazo zimetumika kwa mujibu wa mpango uliowekwa.
Amesema lengo la mradi huo ni kukuza ujuzi, kuongeza ajira na kipato kwa wananchi kupitia ubanguaji wa korosho pamoja na uchakataji wa bidhaa zitokanazo na korosho na mabibo.
Nao baadhi ya vijana 41 wanaojifunza na kufanya kazi katika kiwanda hicho wameishukuru serikali kwa kuwajengea kiwanda hicho, wakisema uwepo wake umewapa fursa ya kujifunza ujuzi na kupata ajira.
Vijana hao wameziomba taasisi nyingine kuongeza jitihada za kuanzisha viwanda vya aina hiyo katika maeneo mbalimbali ili kutoa ajira zaidi na kuongeza kipato cha wananchi.
Mhe. Judith Kapinga,ametembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya za Masasi na Nanyumbu.
Wilayani Masasi, amezindua Kiwanda Darasa cha Kubangua Korosho katika Kijiji cha Mandiwa, amekagua ujenzi wa Ghala la Halmashauri ya Mji Masasi katika eneo la Mtandi, pamoja na kutembelea kiwanda kidogo cha kutengeneza samani cha Vijana Kazi Imara kilichopo Kijiji cha Nanyumbu.
Aidha, Waziri Kapinga ametembelea mradi wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma katika eneo la Masuguru wilayani Nanyumbu, unaotekelezwa chini ya Mamlaka ya Maji ya MANA-WASA.