Jamii FM
Jamii FM
7 September 2026, 18:29

Bodi ya Korosho Tanzania imetangaza kuwa minada rasmi ya mauzo ya korosho kwa msimu wa 2026/2027 itaanza Oktoba 19, huku maandalizi ya msimu huo yakiendelea
Na Musa Mtepa
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Frances Alfred, ametangaza kuwa minada rasmi ya mauzo ya korosho kwa msimu wa 2026/2027 itaanza Oktoba 19, 2026, katika mikoa yote inayolima zao hilo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Septemba 7, 2026, Frances amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Bodi kutekeleza maazimio na maoni yaliyotolewa na wadau wa sekta ya korosho katika mkutano uliofanyika Agosti 27, 2026, mkoani Morogoro.
Amesema maandalizi ya msimu mpya yamekamilika, huku akieleza kuwa kuanzia kesho, Septemba 8, 2026, Bodi itaanza kuweka taarifa mbalimbali kwenye tovuti yake, ikiwemo mchakato wa kuwatambua na kuwahoji waendesha maghala watakaoshiriki katika msimu huo.
Frances amesema waendesha maghala na wadau wengine pia watapatiwa mafunzo maalumu kwa lengo la kuhakikisha taratibu za uhifadhi na usimamizi wa ubora wa korosho zinafuatwa ipasavyo.
Akizungumzia upatikanaji wa magunia ya kuhifadhia korosho, Frances amesema msimu uliopita yalibaki magunia 5,956,000, huku mwaka huu Bodi ikiwa imepokea magunia 7,169,000.
Amesema kwa kujumlisha yaliyobaki kutoka msimu uliopita na yaliyopokelewa mwaka huu, jumla ya magunia yaliyopo ni 13,125,000, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na mahitaji ya magunia 9,375,000 yanayokadiriwa kutumika msimu huu.

Kuhusu soko la awali pamoja na ununuzi na uuzaji wa korosho zinazobanguliwa na wananchi vijijini, Frances amesema Bodi imeanza kuandaa utaratibu maalumu wa kusimamia biashara hiyo.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha korosho zinazozalishwa na kubanguliwa na wananchi zinapata utaratibu mzuri wa uuzaji, huku ubora wa zao hilo ukiendelea kudhibitiwa.
Aidha, Frances amesema kuanza mapema kwa minada ya msimu wa 2026/2027 ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na tahadhari ya uwepo wa mvua za El Niño iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Ameeleza kuwa kuanza kwa minada mapema kutasaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa, huku akiwataka wadau kuchukua tahadhari na kuhakikisha ubora wa korosho unalindwa wakati wote.

Kwa msimu wa 2026/2027, Bodi ya Korosho Tanzania imejiwekea lengo la kuzalisha takribani tani 750,000 za korosho.