Jamii FM

Wakulima na wavuvi Kilambo walia na Daraja la Mtando

26 June 2026, 18:36

Mwonekano wa Daraja la Mtando lililojengwa na Wakulima na Wananchi wanaofanya shughuli za kilimo na uvuvi katika eneo la Mbuyuni/Mwambo Kijiji cha Kilambo (Picha na Musa Mtepa)

Wakulima na wavuvi wa Mbuyuni/Mwambo, Kijiji cha Kilambo mkoani Mtwara, wameiomba Serikali kujenga daraja la kudumu eneo la Mtando ili kurahisisha usafirishaji wa mazao, kuongeza usalama wa watumiaji na kuimarisha shughuli za kiuchumi

Na Musa Mtepa

Wakulima na wavuvi wanaofanya shughuli zao katika eneo la Mbuyuni/Mwambo, Kijiji cha Kilambo, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, wameiomba Serikali kujenga daraja katika eneo la Mtando ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na shughuli nyingine za kiuchumi.

Wakizungumza na Jamii FM Redio, wananchi hao wamesema eneo hilo ni njia muhimu ya kupitisha mazao mbalimbali yanayochangia mapato ya kijiji na Halmashauri kupitia ushuru, hivyo wanaamini ujenzi wa daraja la kudumu utasaidia kuongeza ufanisi wa shughuli za uzalishaji na biashara.

Sauti: Wakulima wa Mbuyuni/Kilambo

Akizungumzia hali ya daraja linalotumika kwa sasa, mkazi na mkulima wa Kijiji cha Kilambo, Mohamedi Dadi Mkoba, amesema daraja hilo limejengwa kwa kutumia miti ambayo huathirika kwa kuoza kadri muda unavyopita, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wake siku zijazo.

Sauti: Mohamedi Dadi Mkoba, mkazi wa Kilambo

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo, Mohamed Ali, amesema suala la daraja hilo liliwahi kujadiliwa katika mikutano ya kijiji na hata kuwasilishwa kwa wataalamu waliofika eneo husika kufanya tathmini na vipimo.

Amesema baada ya tathmini hiyo, wataalamu walieleza kuwa haikuwezekana kutekeleza ujenzi wa daraja hilo kwa kipindi hicho, jambo ambalo limeendelea kuwaacha wananchi wakisubiri utekelezaji wa mradi huo muhimu.

Sauti: Mohamed Ali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo