Jamii FM
Jamii FM
5 July 2026, 13:43

Mtoto mwenye umri wa miaka 13, mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza wa Shule ya Sekondari Mikindani, amefariki baada ya mtumbwi aliokuwa akisafiria kuzama kufuatia upepo mkali katika Bahari ya Hindi, Mtwara
Na Musa Mtepa
Mtoto Mrisho Hassani Nagwenya (13), mkazi wa Mtaa wa Boma, Kata ya Magengeni, Tarafa ya Mikindani, Manispaa ya Mtwara Mikindani, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Mikindani, amefariki dunia baada ya kuzama baharini.
Tukio hilo limetokea Julai 4, 2026, majira ya saa 10:00 jioni katika eneo la Pemba Mvita, Kata ya Naumbu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa marehemu, Mrisho alikuwa ameongozana na wenzake wawili kwenda baharini kutafuta mazao ya baharini aina ya Kumbwa. Hata hivyo, baada ya kushindwa kupata, waliamua kuelekea eneo la Pemba Mvita kutafuta matunda ya kunazi.
Baada ya kumaliza shughuli hiyo, walianza safari ya kurejea nyumbani kwa kutumia mtumbwi. Wakiwa njiani, upepo mkali ulivuma na kuuzamisha mtumbwi waliokuwa wakisafiria, hali iliyosababisha Mrisho kuzama na kupoteza maisha.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnaida, Ismail Mohamedi, amesema alipokea taarifa ya ajali hiyo baada ya kurejea kutoka shambani majira ya saa 1:00 usiku, Amesema wananchi waliinza juhudi za kumtafuta mtoto huyo bila mafanikio, kabla ya kuanza tena operesheni ya utafutaji kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ambapo walifanikiwa kuupata mwili wake ukiwa tayari ameshafariki.

Kwa upande wake, Afisa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Mrakibu Msaidizi Ambrosi Ndunguru, amesema kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vilivyo kandokando ya Bahari ya Hindi katika ukanda wa Mikindani, walifanikiwa kuupata mwili wa Mrisho katika eneo la Pwani ya Pemba, Kata ya Naumbu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao, ikiwemo kujua wanapokwenda na shughuli wanazofanya, ili kupunguza matukio ya ajali kama hayo na kurahisisha utoaji wa msaada wa haraka pale yanapotokea.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mikindani, Mariamu Mohamedi Omari, amethibitisha kupokea mwili wa marehemu na kuthibitisha kifo chake, Amesema mtoto huyo amefariki kutokana na kuzama baharini na kuchelewa kuokolewa, hali iliyosababisha kuingia kwa maji mengi mwilini.