Jamii FM
Jamii FM
2 June 2026, 11:21

Mtwara imekuwa mwenyeji wa mafunzo ya kimataifa ya korosho yaliyowakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 11 za Afrika kujadili mbinu za kuongeza uzalishaji, thamani na masoko ya zao la korosho kwa manufaa ya wakulima na wadau wa sekta hiyo
Na Musa Mtepa
Mkoa wa Mtwara umekuwa mwenyeji wa mafunzo ya kimataifa kuhusu zao la korosho yenye lengo la kubadilishana uzoefu, maarifa na kuimarisha mikakati ya kuongeza thamani ya zao hilo katika nchi mbalimbali za Afrika.
Mafunzo hayo, ambayo hufanyika kila mwaka katika maeneo yanayolima korosho, yanafanyika kwa mara ya pili mfululizo mkoani Mtwara na yamewakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 11 za Afrika kwa lengo la kuendeleza sekta ya korosho barani humo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Donald Msengi, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kubadilishana uzoefu na maarifa yatakayosaidia kuongeza thamani ya zao la korosho na kuboresha maisha ya wakulima kupitia ongezeko la uzalishaji na mapato.
Aidha, Kanal Msengi amesema kufanyika kwa mafunzo hayo mkoani Mtwara ni fursa muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ya mkoa huo, kwani wageni wanaoshiriki hutumia huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi zikiwemo malazi, chakula na usafiri, jambo linalochochea biashara za ndani na kuitangaza Mtwara katika ngazi ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, amesema mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Jukwaa la Korosho Afrika (African Cashew Alliance) yamefanyika Mtwara kutokana na mafanikio makubwa ambayo Tanzania imepata katika sekta ya korosho, hususan katika huduma za ugani na tafiti za kilimo.
Amesema Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine kutokana na mfumo wake wa kuwapeleka vijana wahitimu kutoka vyuoni kuwahudumia wakulima katika maeneo ya vijijini, pamoja na mchango wa tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele katika kuboresha uzalishaji wa korosho.

Naye meneja wa maendeleo ya rasilimali watu Jukwaa la Korosho Afrika( African Cashew Alliance), Reine Dehode, amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa zao la korosho kuanzia uzalishaji shambani, uchakataji hadi upatikanaji wa masoko.
Amebainisha kuwa washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanatumia jukwaa hilo kujifunza mbinu bora za uzalishaji, uchakataji na masoko ya korosho ili kuongeza tija, ubora wa bidhaa na mapato kwa wadau wa sekta hiyo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema yamewapa fursa ya kujifunza teknolojia mpya za uzalishaji wa miche bora ya korosho, mbinu za kuongeza thamani ya zao hilo pamoja na njia za kuboresha masoko, hatua ambazo zinaweza kuongeza faida kwa wakulima na wadau wengine wa sekta ya korosho.
