Jamii FM

Gesi asilia injini ya maendeleo Tanzania

27 April 2026, 16:36

Waziri wa Nishati, Dkt. Deogratius Ndejembi akiwa kwenye ziara mkoani Mtwara na kuzindua bomba la gesi. Picha na Musa Mtepa

Serikali imeendelea kusisitiza ushirikishwaji wa Watanzania katika miradi ya gesi kwa kutoa kipaumbele kwa wataalamu na nguvu kazi ya ndani pia kampuni zinazohusika na miradi hiyo zinahimizwa kutekeleza miradi ya kijamii (CSR) inayolenga kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya na miundombinu katika maeneo yanayozunguka miradi hiyo.

Na Musa Mtepa

Tanzania inaendelea kunufaika na utajiri mkubwa wa gesi asilia, ikiwa na zaidi ya futi za ujazo trilioni 57. Rasilimali hii imekuwa mhimili wa uzalishaji wa umeme, ambapo zaidi ya asilimia 50 ya nishati ya umeme nchini inatokana na gesi.

Maeneo ya kusini hasa Mtwara na Lindi ndiyo kitovu cha uzalishaji, kupitia vitalu vya Mnazi Bay na Songo Songo. Hata hivyo, matumaini mapya yanaibukia Ntorya, ambako zaidi ya futi trilioni 1.6 za gesi zimegunduliwa, zikitarajiwa kuongeza uzalishaji.

Moja ya mtambo uliopo Msimbati mkoani Mtwara. Picha na Musa Mtepa

Mnamo Februari 27–28, 2026, Waziri wa Nishati, Dkt. Deogratius Ndejembi, alifanya ziara mkoani Mtwara na kuzindua bomba la gesi la kilomita 34.2 kutoka Ntorya hadi Madimba hatua muhimu ya kuimarisha miundombinu ya nishati.

Serikali inalenga kufikia uzalishaji wa megawati 8,000 za umeme ifikapo 2030, huku uwekezaji mkubwa ukiendelea katika miradi ya gesi. Katika Mnazi Bay, uchimbaji wa visima vipya unaendelea kuongeza uzalishaji.

Mbali na hilo, tafiti za kisasa za 3D seismic zinaendelea Lindi na Mtwara kubaini rasilimali zaidi, huku serikali ikisisitiza ushirikishwaji wa Watanzania na utekelezaji wa miradi ya kijamii (CSR).

Kusikiliza kipindi hiki, Bonyeza hapa