Jamii FM

Ndejembi awasha umeme Sekondari, Mtwara

23 July 2026, 14:29

Waziri wa Nishati Mhe. Ndejembi akiwasha umeme katika Shule ya Sekondari Mtiniko iliyopo halmashauri ya Mji Nanyamba,Mkoani Mtwara. Picha na Musa Mtepa

Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi amewasha umeme katika Shule ya Sekondari Mtiniko, Nanyamba, na kusema Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 203 kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji vya Mkoa wa Mtwara

Na Musa Mtepa

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, Julai 21, 2026 amewasha umeme katika Shule ya Sekondari Mtiniko iliyopo Kitongoji cha Maendeleo, Kata ya Mtiniko, Halmashauri ya Mji Nanyamba ikiwa ni cha 314 kati ya vitongoji 324 vilivyofikiwa na huduma ya umeme katika halmashauri hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uwashaji wa umeme huo, Waziri Ndejembi amesema kufikishwa kwa umeme katika shule hiyo kunatokana na jitihada za Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Mhe. Abdalla Dadi Chikota, ambaye alichagua eneo hilo baada ya Serikali kutoa fursa ya kupeleka umeme katika vitongoji kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Sauti: Deogratius Ndejembi – Waziri wa Nishati

Waziri Ndejembi amesema Serikali imepeleka zaidi ya Shilingi bilioni 203 mkoani Mtwara kwa ajili ya kukamilisha miradi ya kusambaza umeme katika vijiji na vitongoji. Kati ya fedha hizo, Jimbo la Nanyamba limepokea Shilingi bilioni 6.9, zilizowezesha kupeleka umeme katika vijiji vyote 87 na vitongoji 306 kati ya 324.

Sauti: Deogratius Ndejembi – Waziri wa Nishati

Aidha, Waziri amesema Serikali inaendelea kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 Tanzania inazalisha megawati 8,000 za umeme, ikilinganishwa na takribani megawati 4,000 zinazozalishwa kwa sasa.

Sauti: Deogratius Ndejembi – Waziri wa Nishati

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amewataka wananchi kuendelea kulinda na kutunza miundombinu ya nishati na barabara ili iweze kutoa manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.


Sauti: Kanali Donald Msengi – Mkuu wa Mkoa wa Mtwara

Naye Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Mhe. Abdalla Dadi Chikota, ameishukuru Serikali na Waziri wa Nishati kwa kuhakikisha vijiji vyote 87 vya jimbo hilo vinafikiwa na huduma ya umeme, hatua aliyosema itachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Sauti: Abdalla Dadi Chikota – Mbunge wa Jimbo la Nanyamba