Jamii FM
Jamii FM
3 September 2026, 08:46

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewataka wananchi kushiriki Tamasha la Nyangumi, likilenga kukuza utalii wa baharini, uhifadhi wa mazingira na fursa za kiuchumi kwa jamii
Na Grace Hamisi
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki Tamasha la Nyangumi, linaloanza leo Septemba 3, 2026 na kufikia kilele chake Septemba 5, mwaka huu.
Mwaipaya ametoa wito huo jana, Septemba 2, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo amesema tamasha hilo ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuitangaza Mtwara kupitia utalii wa baharini.
Amesema uwepo wa nyangumi katika maeneo ya bahari ya Mtwara ni fursa inayoweza kuchochea ukuaji wa utalii wa kiikolojia, huku wananchi wakipata uelewa zaidi kuhusu umuhimu wa kutunza bahari na viumbe wanaoishi ndani yake.
Aidha, amesema kupitia tamasha hilo, wananchi na wageni watapata fursa ya kufahamu zaidi kuhusu nyangumi na namna uwepo wa viumbe hao unavyoweza kuwa chanzo cha fursa za kiuchumi kwa jamii.

Kwa upande wake, Muhifadhi Mfawidhi wa Hifadhi ya Ghuba ya Mnazi Bay, Redfrey Ngowo, amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wamekuwa wakihamasisha jamii kuelewa uwepo wa nyangumi na namna rasilimali hiyo inavyoweza kutumika kama fursa ya utalii.
Ngowo amesema hatua hiyo pia inalenga kuwavutia wawekezaji kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii wa nyangumi.

Naye Meneja wa Mradi wa Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu, Remmy Lema, amesema tamasha hilo limejikita katika kufungua fursa za utalii kwa Kanda ya Kusini, sambamba na kuwajengea uwezo wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza na kulinda ikolojia ya eneo hilo.
Lema amesema ushiriki wa jamii ni muhimu ili kuhakikisha fursa za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa nyangumi zinaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira ya bahari.