Jamii FM

Ndejembi akerwa na kasi ndogo ya miradi ya TACTICS Mtwara

13 November 2026, 16:45

Makamu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa maagizo kwa mkandarasi anaetekeleza mradi wa TACTICS Manispaa ya Mtwara Mikindani (Picha na Musa Mtepa)

Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi amemtaka mkandarasi wa miradi ya TACTICS Mtwara kukamilisha kazi ifikapo Machi 2027, akionya kuchukuliwa hatua za kisheria endapo atashindwa kutekeleza wajibu wake

Na Musa Mtepa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amemtaka mkandarasi anayetekeleza miradi ya TACTICS katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ifikapo Machi Mosi, 2027, akionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa endapo atashindwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati.

Ametoa agizo hilo leo, Novemba 13, 2026, alipotembelea mradi wa ujenzi wa soko la wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga, unaotekelezwa katika eneo la Skoya, na kueleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Sauti ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi.

 Mhe. Ndejembi amemtaka mkandarasi huyo kama hana uwezo wa kukamilisha mradi kwa wakati kutafuta mkandarasi mwingine mwenye uwezo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unapaswa kuzingatia masharti ya mkataba, huku akionya kuwa serikali haitavumilia hali ya kutokuwepo kwa ongezeko la kasi ya utekelezaji.

Sauti ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi

Kwa upande wao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Wilson Msengi, wamesema hawajaridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Wamesema hali hiyo imewalazimu kupanga kukutana na mkandarasi ili apate kutoa maelezo kuhusu sababu za kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi hiyo na hatua atakazochukua kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Sauti za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Wilson Msengi

Awali, kabla ya Makamu wa Rais kutoa maagizo hayo, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Mhe. Dkt. Joel Nanauka, alimuomba Makamu wa Rais kutoa maelekezo kuhusu hali ya utekelezaji wa mradi huo ili kuharakisha ukamilishaji wake na kuhakikisha unakamilika kwa wakati.

Sauti ya Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Mhe. Dkt. Joel Nanauka

Miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania, TACTICS, inayotekelezwa katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ina thamani ya shilingi bilioni 27.49.

Miradi hiyo inahusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali, ikiwemo barabara ya Chuno yenye urefu wa kilomita 3.38, barabara ya Samia City Access yenye urefu wa kilomita 2.4, ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua eneo la Kiyangu yenye urefu wa kilomita 1.73, kituo cha wajasiriamali wadogo eneo la Skoya, pamoja na kituo kikuu cha mabasi eneo la Chipuputa.

Miradi hiyo inatekelezwa na kampuni ya M/S Serengeti Limited, kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania kupitia mkopo wa Benki ya Dunia, ikiwa na lengo la kuboresha miundombinu ya mji na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.