Jamii FM

Bodi ya Korosho yatakiwa kudhibiti ubadhirifu wa fedha za wakulima

13 November 2026, 18:48

Makamu wa Rais Mhe.Ndejembi akichota Korosho kwa ajili ya kuweka kwenye mashine za kubangulia korosho baada ya kuweka jiwe la msingi katika kongani la viwanda Maranje(Picha na Musa Mtepa)

Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi ameitaka Bodi ya Korosho Tanzania kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika mkoani Mtwara ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha na kulinda maslahi ya wakulima

Na Musa Mtepa

Bodi ya Korosho Tanzania imetakiwa kuongeza usimamizi na ufuatiliaji wa vyama vikuu vya ushirika vinavyoshughulika na zao la korosho mkoani Mtwara ili kubaini na kudhibiti malalamiko ya matumizi mabaya ya fedha yanayowasilishwa na wakulima.

Wito huo umetolewa leo Novemba 13, 2026 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati wa hafla ya kukabidhi mashine za kubangua korosho, iliyofanyika baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda iliyopo kijiji cha Maranje, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba.

Mhe. Ndejembi amesema amepokea taarifa za kuwepo kwa malalamiko kuhusu fedha zinazotengwa na vyama hivyo kwa ajili ya matumizi mbalimbali, lakini baadaye kutoweka bila maelezo ya wazi, hali inayozua maswali kuhusu uwajibikaji wa viongozi wa vyama hivyo na usimamizi wa rasilimali zinazopaswa kuwanufaisha wakulima.

Sauti ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi
default

Aidha, Makamu wa Rais amesema Serikali kuu itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mtwara kuhakikisha Kongani ya Viwanda inawekewa miundombinu muhimu itakayowezesha kufikia malengo ya kuwa kitovu cha uzalishaji viwandani kwa Mkoa wa Mtwara na ukanda wa Kusini kwa ujumla, ikiwemo upatikanaji wa umeme wa uhakika na gesi asilia.

Sauti ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amewapa pole wakulima wa korosho kutokana na changamoto iliyojitokeza katika uzalishaji wa zao hilo msimu huu, huku akieleza kuwa Serikali itafuatilia na kubaini sababu zilizosababisha uzalishaji kutofikia matarajio ya awali.

Sauti ya Daniel Chongolo, Waziri wa Kilimo

Naye Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdala Dadi Chikota, amesema uwepo wa Kongani ya Viwanda utachochea fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitia ajira, kuongeza mapato ya halmashauri kutokana na kodi na kupanua soko la korosho, jambo litakaloweza kuongeza ushindani na bei ya zao hilo kwa wakulima.

Sauti ya Abdala Dadi Chikota, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba