Jamii FM
Jamii FM
23 October 2026, 22:25

Wakulima wa korosho nchini watakiwa kuzingatia ukaushaji na uhifadhi sahihi wa zao hilo ili kulinda ubora na kupunguza gharama za vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS)
Na Musa Mtepa
Wakulima wa zao la korosho nchini wametakiwa kuhakikisha wanazianika na kuzikausha vizuri korosho zao wakiwa nyumbani kabla ya kuzipeleka ghalani, hatua itakayosaidia kupunguza gharama kwa vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) za kuanika upya korosho zisizokauka ipasavyo.
Wito huo umetolewa Oktoba 22, 2026 na Desdery Karugaba, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi kutoka Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio Mtwara.
Amesema baadhi ya wakulima wamekuwa na tabia ya kupeleka korosho ghalani bila kuzianika vizuri wakiwa nyumbani, hali inayosababisha vyama vya msingi vya ushirika kuingia gharama za ziada za kuzianika upya.
Aidha, amevitaka vyama vya ushirika (AMCOS) kuzingatia ubora wa korosho wakati wa mapokezi na kutopokea korosho ambazo hazijakaushwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake, Jamali Akida, Afisa Udhibiti Ubora kutoka CBT, amewasisitiza wakulima kuzingatia njia sahihi za kuhifadhi korosho kwa kutumia vifungashio vinavyofaa.
Amesema endapo mkulima hana vifungashio vinavyostahili, anaweza kutengeneza kichanja maalumu cha kuhifadhia korosho ili ziweze kupata hewa ya kutosha na kulinda ubora wake kabla ya kupata Magunia.
Aidha, Jamali amesema kuzingatia viwango vya ubora wa korosho kunaongeza uwezekano wa wakulima kupata bei nzuri, kwa kuwa wanunuzi huvutiwa na korosho zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Ameongeza kuwa taarifa za ubora wa korosho zilizopo maghalani huwasaidia wanunuzi kufanya maamuzi ya kununua mzigo husika.
