Jamii FM
Jamii FM
28 October 2026, 12:19

Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, azindua ugunduzi wa gesi wenye futi za ujazo bilioni 223 katika kisima cha Kasa 1X, Mnazi Bay, mkoani Mtwara
Na Musa Mtepa
Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, amezindua ugunduzi mpya wa gesi asilia katika kitalu cha Mnazi Bay, kupitia kisima cha Kasa 1X, kinachokadiriwa kuwa na futi za ujazo bilioni 223 za gesi asilia.
Akizungumza na wananchi wa Msimbati baada ya uzinduzi huo jana Oktoba 27, 2026, Dkt. Homera amesema kisima hicho kinatarajiwa kuzalisha futi za ujazo milioni 30 za gesi kwa siku kwa kipindi kisichopungua miaka 10. Hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa gesi asilia na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla.
Ameipongeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na kampuni mshirika ya M&P kwa uamuzi wa kuwekeza katika mradi huo, akisema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo sekta ya nishati.

Aidha, Dkt. Homera amesema ugunduzi huo unatarajiwa kuleta manufaa mbalimbali, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa umeme, kuimarisha usalama wa nishati na kuvutia uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji wa salfa na mbolea.
Ameongeza kuwa mradi huo utaongeza mapato ya Serikali na halmashauri kupitia shughuli za uzalishaji na uwajibikaji kwa jamii (CSR), yatakayosaidia kutekeleza miradi ya maendeleo na kufanikisha azma ya Tanzania kuwa nchi yenye viwanda vingi ifikapo mwaka 2050.
Katika hatua nyingine, Waziri Homera amesema Serikali inaendelea na operesheni ya kuhakikisha umeme unawashwa katika vijiji na vitongoji vyote nchini kupitia wakala wa nishati vijijini (REA), kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa na wilaya, ili kila Mtanzania aweze kuishi katika nyumba yenye huduma ya umeme.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, ameiomba Serikali kuzingatia changamoto za wananchi wa Msimbati kuhusu miundombinu ya barabara na upatikanaji wa umeme, pamoja na kilio cha wakazi wa Mtwara kwa ujumla kuhusu kuunganishiwa huduma ya gesi asilia majumbani.

Uzinduzi huo ni sehemu ya ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Nishati mkoani Mtwara, ambapo pia alitembelea eneo la maungio ya bomba la gesi kutoka kisima cha Ntorya-1, kata ya Nanguruwe, lenye urefu wa kilomita 35 kuelekea kituo cha kuchakata gesi asilia cha Madimba.
Baada ya ziara hiyo, alizindua ugunduzi mpya wa gesi katika kisima cha Kasa 1X, kilichopo kata ya Msimbati, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Kisima hicho kikikamilika kwa asilimia 100 na kuanza uzalishaji, kinatarajiwa kuongeza idadi ya visima vya gesi asilia katika kata ya Msimbati kufikia vinane, huku utafiti wa rasilimali hiyo ukiendelea katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja na maeneo mengine nchini.