Jamii FM
Jamii FM
16 October 2026, 13:04

Kipindi maalumu kinachojadili utunzaji wa mazingira na tahadhari dhidi ya athari za mvua za El Niño, kupitia mahojiano na maafisa wa NEMC Kanda ya Kusini.
Na Musa Mtepa
Karibu katika kipindi hiki maalumu kinachozungumzia utunzaji wa mazingira na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri kuanza kwa mvua za msimu wa vuli zinazohusishwa na athari za El Niño katika baadhi ya maeneo nchini kuanzia mwishoni mwa Septemba hadi mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa utabiri huo, mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika maeneo ya ukanda wa ziwa Victoria kabla ya kusambaa taratibu katika maeneo mengine yanayopata mvua za Vuli.
TMA inaeleza kuwa kiwango cha mvua kinatarajiwa kuongezeka zaidi mwezi Novemba 2026, huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kuendelea kupata mvua hadi Januari 2027.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wanahimizwa kuchukua tahadhari mapema kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, kusafisha mifereji ya maji, kuepuka kutupa taka katika vyanzo vya maji na kuzingatia maelekezo ya mamlaka husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza, ikiwemo mafuriko na uharibifu wa mali na miundombinu.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata elimu na taarifa sahihi kuhusu utunzaji wa mazingira pamoja na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana na athari za mvua hizo, Jamii FM Radio imefanya mahojiano maalumu na maafisa kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kanda ya Kusini.
Katika mahojiano hayo, utamsikia Magori Wambura, Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC Kanda ya Kusini, pamoja na Ramadhani Juma, Afisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC Kanda ya Kusini, wakieleza umuhimu wa utunzaji wa mazingira na hatua za kuchukua kabla, wakati na baada ya mvua hizo.