Jamii FM

Kongani la Maranje kuchochea upandaji wa bei ya korosho

14 November 2026, 20:06

Mwonekano wa juu wa eneo la Kongoni la Viwanda vya ubanguaji Korosho linalojengwa katika kijiji cha Maranje halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara

Mkurugenzi wa WRRB, Asangye Bangu, amesema uwepo wa Kongani la Viwanda Maranje utaongeza ushindani katika soko la korosho na kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri kupitia ubanguaji wa zao hilo nchini.

Na Musa Mtepa

Uwepo wa Kongani la Viwanda katika Kijiji cha Maranje unatajwa kuwa kichocheo muhimu cha kuongeza ushindani na kupandisha bei ya korosho, hatua inayolenga kuongeza manufaa kwa wakulima wa zao hilo nchini.

Hayo yamesemwa Novemba 13, 2026 na Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la Kongani la Viwanda la Maranje uliofanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bangu amesema kuongezeka kwa viwanda vya kubangua korosho kutatoa fursa kwa wakulima kupata bei nzuri zaidi kupitia mfumo wa stakabadhi za ghala, kwa kuwa wanunuzi na wawekezaji watakuwa karibu na maeneo ya uzalishaji, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Sauti ya Asangye Bangu, Mkurugenzi wa WRRB

Akizungumzia ongezeko la maghala ya kuhifadhi korosho, Bangu amesema hali hiyo ni ishara ya kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo na mahitaji ya nafasi za kutosha za kuhifadhi korosho zinazozalishwa na wakulima.

Ameongeza kuwa uwepo wa maghala mengi ni fursa kwa wakulima, huku akisisitiza kuwa maghala yanayojengwa yanapaswa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa akisistiza WRRB haitoi leseni kwa maghala ambayo hayakidhi viwango vilivyowekwa.

Sauti ya Asangye Bangu, Mkurugenzi wa WRRB

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Frances Alfred, amesema kukamilika kwa Kongani hilo kwa asilimia 100 kunatarajiwa kuwezesha kubanguliwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya korosho zinazozalishwa nchini ifikapo mwaka 2030.

Amesema mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi Bilioni 343.4, huku wawekezaji wawili wakiwa tayari wameanza maandalizi ya kujenga viwanda viwili katika eneo hilo, vinavyotarajiwa kuwa na uwezo wa kubangua tani 250,000 za korosho ghafi.

Sauti ya Frances Alfred, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT)