Jamii FM

Balozi wa Finland aipa 5 Jamii FM inavyohudumia jamii

20 October 2026, 11:38

Balozi wa Finland Anna Merrifiel akisalimiana na mwenyekiti wa Mtu kwao Community Media inayomiliki Jamii fm Redio ambae pia ni miongoni mwa wamiliki Fakihi Musa Mnanambula alipotembelea kituo hicho jana Oktoba 19, 2026 .(Picha na Henri Chivihi)

Balozi wa Finland nchini Tanzania Anna Merrifield ameitembelea redio Jamii FM ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano uliopo hasa katika vipindi vya wanawake, mazingira na watu wenye ulemavu.

Na Musa Mtepa

Balozi wa Finland nchini Tanzania, Anna Merrifield, ameipongeza Jamii FM Radio kwa mchango wake katika kuhabarisha wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi, pamoja na kuwa kiungo kati ya jamii na viongozi wa serikali.

Balozi Merrifield ametoa pongezi hizo Oktoba 19, 2026, alipotembelea kituo hicho kilichopo Kata ya Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, akisema redio hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuibua na kujadili masuala mbalimbali ya kijamii, yakiwemo haki za wanawake, utunzaji wa mazingira na masuala ya watu wenye ulemavu.

Sauti ya Balozi Anna Merrifield

Aidha, Balozi Merrifield amesema ana matumaini kuwa Jamii FM itaendelea kutumia vipindi vyake kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na kuimarisha mawasiliano kati ya jamii na viongozi wa serikali.

Sauti ya Balozi Anna Merrifield

Akizungumzia kiwango cha wanawake wenye elimu ya juu nchini Finland ikilinganishwa na Tanzania, Balozi Merrifield amesema si Finland pekee inayopiga hatua katika elimu ya wanawake, bali pia Tanzania ina wanawake wengi waliofanikiwa kufikia elimu ya juu.

Ametolea mfano mahafali yaliyofanyika hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akisema zaidi ya asilimia 50 ya wahitimu walikuwa wanawake.

Sauti ya Balozi Anna Merrifield

Katika hatua nyingine, Balozi Merrifield amesema Mtwara imekuwa mkoa wake wa kwanza kutembelea tangu alipoteuliwa kuwa Balozi wa Finland nchini Tanzania, kutokana na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Finland na Mtwara ulioanza tangu miaka ya 1980.

Amesema ushirikiano huo umejikita katika maeneo mbalimbali, ikiwemo miradi ya maji na sekta ya habari kupitia ushirikiano wa muda mrefu kati ya Jamii FM Radio na shirika la VIKES.

Sauti ya Balozi Anna Merrifield