Jamii FM

BMU Namela yatoa msaada kwa jamii ya Msangamkuu

6 November 2026, 08:00

Katibu msaidizi wa BMU kijiji cha Namela Maafudhi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi vifaa hivyo(Picha na Shaibu Omari)

BMU Namela imetoa msaada wa vifaa vya elimu, sare za shule na vyakula kwa jamii ya Msangamkuu, ikiwa ni sehemu ya mrejesho wa ushirikiano katika uhifadhi wa rasilimali za bahari na pwani

Na Shaibu Omari

Kikundi cha usimamizi shirikishi wa rasilimali za Bahari na Pwani (BMU) cha Namela, kilichopo kata ya Msangamkuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, kimetoa msaada wa vifaa vya elimu, sare za shule na vyakula kwa jamii ya kata hiyo.

Msaada huo uliotolewa Novemba 4, 2026, ni sehemu ya mrejesho wa kikundi hicho kwa jamii inayokishirikiana nacho katika shughuli za uhifadhi na ulinzi wa mazingira ya bahari na pwani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Katibu Msaidizi wa BMU Namela, Maafudhi Alli Ahmadi, amesema wameamua kuirudishia jamii sehemu ya manufaa yanayotokana na ushirikiano wao katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.

Amesema msaada huo umejumuisha kilogramu 50 za unga, kilogramu mbili za sukari, sare za shule kwa wanafunzi sita wa Shule ya Msingi Msangamkuu, pamoja na juzuu 450 kwa madrasa tisa zilizopo katika kata hiyo.

Sauti ya Maafudhi Alli Ahmadi, Katibu Msaidizi wa BMU Namela.

Aidha, Maafudhi ameiomba Serikali na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi hizo ili kuongeza wigo wa misaada kwa jamii, hususan katika sekta ya elimu.

Sauti ya Maafudhi Alli Ahmadi, Katibu Msaidizi wa BMU Namela

Kwa upande wake, Afisa Uvuvi wa Wilaya ya Mtwara, Juliana Msemwa, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na BMU katika kulinda na kutunza rasilimali za bahari na pwani, akisema juhudi hizo zina manufaa ya moja kwa moja kwa jamii, ikiwemo upatikanaji wa misaada mbalimbali.

Sauti ya Juliana Msemwa, Afisa Uvuvi Wilaya ya Mtwara

Naye, Ostadhi wa Madrasa ya Almadrasati, Shababy Abdukarim Yusufu, pamoja na Afisa Elimu wa kata ya Msangamkuu, Mwalimu Ismaili Likwembe, wameipongeza BMU Namela kwa msaada huo, wakisema utasaidia kuboresha shughuli za elimu.

Viongozi hao pia wamewataka wananchi kuendelea kushirikiana na kikundi hicho katika shughuli zake za uhifadhi wa rasilimali za bahari na pwani.

Sauti za Ostadhi Abdukarim na Mwalimu Likwembe

Nao wanafunzi wa Shule ya Sekondari Msangamkuu wameishukuru BMU Namela kwa msaada wa chakula na sare za shule, wakisema utawasaidia katika mahitaji yao ya kielimu.

Sauti za wanafunzi wa Shule ya Sekondari Msangamkuu

.