Jamii FM

Mtoto wa miaka 13 adaiwa kuozeshwa mkoani Lindi

26 November 2026, 18:16

Picha kwa msaada wa mtandao ikionesha tukio la ufungaji ndoa

Mtoto anayekadiriwa kuwa na miaka 13 anadaiwa kuozeshwa Lindi, huku tukio hilo likizua maswali kuhusu ndoa za utotoni, wajibu wa wazazi na ulinzi wa haki za mtoto

Na Musa Mtepa

Mtoto Shailuni Ashrafu Chalido, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 13, mkazi wa Ngongo, mkoani Lindi, anadaiwa kuozeshwa katika mazingira ya siri, Novemba 25, 2026, baada ya majirani kuhoji umri wake.

Wakizungumza na kituo cha redio cha Mashujaa mkoani humo, baadhi ya wananchi wamesema mtoto huyo aliacha shule mwaka 2025 akiwa darasa la sita, huku sababu za kuacha masomo zikiwa hazijafahamika kwa wakati huo.

Aidha, wananchi hao wanadai kuwa mtoto huyo ameozeshwa kwa mwanaume mwenye umri mkubwa anayeishi Dar es Salaam, kwa ridhaa ya wazazi wake, ambapo mwanaume huyo alimtuma mwakilishi kwa ajili ya kufanikisha taratibu za ndoa.

Sauti za wananchi na majirani wa familia hiyo, Ngongo

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngongo amesema hakuwa na taarifa za maandalizi ya ndoa hiyo hadi alipopata taarifa kutoka kwa wananchi, ndipo alipofika eneo la tukio na kumkuta mtoto huyo akiwa amepambwa kwa mavazi ya harusi.

Mwenyekiti huyo amesema licha ya ndoa hiyo kuripotiwa kufungwa Novemba 25, 2026, anatarajia kuwakutanisha wazazi wa pande zote mbili ili kubaini mazingira ya tukio hilo na hatua zilizochukuliwa.

Sauti ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngongo

Katika hatua nyingine, Jamii FM Radio ya Mtwara ilifanya jitihada za kumtafuta Ashrafu Chalido, baba mzazi wa mtoto huyo, mkazi wa Kijiji cha Lideko, mkoani Lindi, ambaye amethibitisha kumwozesha binti yake, huku akikiri kuwa mtoto huyo kwa sasa si mwanafunzi.

Akielezea sababu za mtoto huyo kuacha shule, Chalido amesema alifanya jitihada mbalimbali za kumshawishi aendelee na masomo hadi kumaliza darasa la saba, lakini hakufanikiwa kutokana na kile alichodai kuwa mtoto huyo hakuwa tayari kuendelea na masomo na badala yake alitamani kujifunza ufundi wa kushona nguo.

Sauti ya Ashrafu Chalido, baba mzazi wa mtoto huyo

Akizungumzia mazingira ya ndoa hiyo, Chalido amesema alipata taarifa kutoka kwa mama mzazi wa mtoto huyo, ambaye alikuwa akiishi naye Ngongo, kuwa binti yake amepata mchumba anayehitaji kumuoa.

Amesema baada ya kupata taarifa hizo, alizungumza mwenyewe na binti yake ili kujiridhisha, ambapo alidai mtoto huyo alimweleza kuwa amepata mchumba na hakuwa amelazimishwa kuolewa na mtu yeyote.

Chalido amesema baada ya mazungumzo hayo alitoa ridhaa yake na taratibu za ndoa hiyo zikafanyika Novemba 25, 2026, katika Kijiji cha Lideko.

Sauti ya Ashrafu Chalido, baba mzazi wa mtoto huyo

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Lideko, Salumu Issa Mwambusi, amethibitisha kufungwa kwa ndoa hiyo katika kijiji hicho, akisema kuwa ni tukio la tatu analolishuhudia katika eneo hilo linalohusisha watoto wenye umri kati ya miaka 12 na 14 kuozeshwa.

Mwambusi amedai kuwa baadhi ya sababu zinazochangia matukio hayo ni ukosefu wa uelewa wa sheria miongoni mwa wananchi pamoja na hali ngumu ya kiuchumi inayokabili familia nyingi katika maeneo hayo.

Sauti ya Salumu Issa Mwambusi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lideko