Jamii FM
Jamii FM
23 October 2026, 18:26

Benki ya NMB yazindua kampeni kwa wadau wa korosho ukanda wa kusini, ambapo wakulima, wafanyabiashara na vyama vya ushirika watapata nafasi ya kujishindia trekta kupitia mauzo yao
Na Musa Mtepa
Benki ya NMB leo Oktoba 23, 2026, imezindua kampeni maalumu kwa wadau wa biashara ya korosho, inayolenga wakulima, wafanyabiashara na vyama vikuu vya ushirika vinavyopitisha malipo ya mauzo ya korosho kupitia akaunti za benki hiyo, ambapo mshindi wa kampeni hiyo atajishindia trekta.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, ameitaka Benki ya NMB kwa kushirikiana na kampuni ya CMC kutoa elimu kwa viongozi wa vyama vya ushirika na wakulima ili waelewe namna kampeni hiyo itakavyowanufaisha.

Akielezea kampeni hiyo, Mkuu wa Matawi na Mauzo wa Benki ya NMB, Donatus Richard, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya kuwahamasisha wadau wa korosho kutumia huduma za benki hiyo, huku ikitoa motisha kwa vyama vikuu vya ushirika, wakulima na wafanyabiashara kujishindia trekta.
Amesema ili wadau hao kuongeza nafasi ya kushinda zawadi hiyo, wanapaswa kuhakikisha wanapitisha wastani wa asilimia 60 au zaidi ya malipo ya mauzo yao ya korosho kupitia akaunti za Benki ya NMB.

Kwa upande wao, viongozi wa vyama vikuu vya ushirika vya TANECU na MAMCU, Hadija Hassani Mpinga, Makamu Mwenyekiti wa TANECU, pamoja na Alhaji Azam Mfaume, Mwenyekiti wa MAMCU, wameipongeza Benki ya NMB kwa kuanzisha kampeni hiyo.
Viongozi hao wameahidi kushirikiana na benki hiyo kwa kuhakikisha malipo ya mauzo ya korosho yanapitia akaunti za NMB ili kuongeza nafasi ya vyama vyao kujishindia trekta litakalotolewa kupitia kampeni hiyo.

Kampeni hiyo inalenga wadau wa biashara ya korosho katika ukanda wa kusini, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara na vyama vikuu vya ushirika, wanaotumia akaunti za Benki ya NMB kupitisha malipo ya mauzo ya zao hilo, huku mshindi akitarajiwa kujinyakulia trekta.