Jamii FM
Jamii FM
19 November 2026, 08:14

Wananchi wa Maranje wameeleza matumaini ya kupata ajira na fursa za kiuchumi kupitia Kongani ya Viwanda, huku viwanda 30 vikitarajiwa kujengwa katika eneo hilo
Na Musa Mtepa
Wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka kongani ya viwanda ya Maranje, wilayani Mtwara, wameeleza matumaini yao kuwa uwepo wa kongani hiyo utaongeza thamani ya zao la korosho nchini, sambamba na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi.
Wakizungumza na Jamii FM Radio, wananchi hao wamesema uwepo wa viwanda hivyo utachochea upatikanaji wa ajira na shughuli za kujipatia kipato, ikiwemo biashara za mama lishe, huduma za usafiri wa bodaboda pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi.
Kwa upande wake, Pius Kabaka, mkazi wa kijiji cha Maranje, ameipongeza Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa viwanda katika eneo hilo, huku akiwahimiza wananchi kutumia fursa zinazotokana na uwepo wa kongani hiyo kwa kuwekeza katika elimu ya watoto wao na kuboresha makazi yao ili yaweze kuvutia wafanyakazi wa viwandani kupata sehemu za kupanga.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdala Dadi Chikota, amewashukuru wananchi wa kijiji cha Maranje kwa kuridhia kutoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kongani hiyo, huku akiipongeza Bodi ya Korosho Tanzania kwa kusimamia ujenzi wa viwanda katika eneo hilo.
Akizungumzia matarajio ya uwekezaji katika kongani hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Frances Alfred, amesema jumla ya viwanda 30 vinatarajiwa kujengwa katika eneo hilo, idadi ambayo inaweza kuongezeka kulingana na ukubwa wa viwanda na mahitaji ya wawekezaji.
.