Jamii FM

Serikali yaipa TIRA jukumu la kudhibiti kampuni za bima

23 October 2026, 08:01

Waziri Mchengerwa na baadhi ya viongozi wa serikali wakiwasha mishumaa ishara ya uzinduzi rasmi wa awamu ya pili wa dirisha la usajili wa bima ya afya kwa wote(Picha na Musa Mtepa)

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, aitaka TIRA kusimamia kampuni za bima na kulinda michango ya wananchi wakati Mtwara ikiweka lengo la kusajili wananchi 51,943 katika awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote

Na Musa Mtepa

Serikali imeitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kusimamia kikamilifu kampuni zote zinazotoa huduma za bima nchini na kuchukua hatua dhidi ya kampuni zinazobainika kufanya udanganyifu au kukiuka masharti ya mikataba, ikiwemo kuzifutia mikataba pale inapobidi, ili kulinda maslahi ya wananchi na misingi ya Bima ya Afya kwa Wote.

Wito huo umetolewa jana, Oktoba 22, 2026, na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati wa uzinduzi wa dirisha la usajili wa awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote, uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba, Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.

Amesema TIRA ina wajibu wa kusimamia soko la bima nchini kwa kuhakikisha watoa huduma za bima wanatunza michango ya wananchi na kuzingatia masharti ya mikataba, huku hatua stahiki zikichukuliwa dhidi ya kampuni zinazokiuka taratibu.

Sauti ya Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Afya

Sambamba na hilo, Waziri Mchengerwa amewataka wananchi kujiandikisha mapema katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote badala ya kusubiri kuugua ndipo wafikirie kujiunga na huduma za bima.

Amesema kila mwananchi ana wajibu wa kuhamasisha wengine kujiunga na bima ya afya ili kujikinga na gharama kubwa za matibabu ambazo zinaweza kuepukika kupitia huduma hiyo.

Sauti ya Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Afya

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Said Nyengedi, amewataka wahudumu wa afya kutoa huduma bora na zenye staha, kuwapokea wagonjwa kwa uchangamfu na kuhakikisha wanapata huduma bila kubaguliwa kwa kuzingatia aina ya bima waliyonayo.

Sauti ya Said Nyengedi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Wilson Msengi, ameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhamasisha wananchi wanaostahili kujiunga na mpango huo katika awamu hii ya pili.

Amesema mkoa umeweka lengo la kusajili jumla ya wananchi 51,943 kutoka katika kaya 28,918.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara

Nao baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Mtwara wameipongeza Serikali kwa kuzindua dirisha hilo la usajili, huku wakiahidi kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Sauti ya baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Mtwara

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wameipongeza Serikali kwa kuanzisha mpango huo, wakisema utawasaidia kupata huduma za afya na kupunguza gharama za matibabu, huku wakiahidi kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi wengine kujiunga na bima hiyo.

Sauti ya baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo.