Jamii FM

Makamu wa Rais aweka jiwe la msingi mradi wa maji wa miji 28 Mtwara

12 November 2026, 22:42

Makamu wa Rais Mhe. Deogratius Ndejembi akiweka jiwe la msingi katika mradi wa kutooa maji mto Ruvuma katika kijiji cha Masuguru wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara

Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa miji 28 wenye thamani ya shilingi bilioni 38 katika kijiji cha Masuguru, Nanyumbu mkoani Mtwara, unaolenga kuondoa changamoto ya maji na hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali

Na Musa Mtepa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, leo Novemba 12, 2026, ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa miji 28 katika kijiji cha Masuguru, kata ya Masuguru, Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.

Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 38, unaotekelezwa chini ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Masasi–Nachingwea (MANAWASA), unatarajiwa kuhudumia miji 28 na kuwaondolea wananchi changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, pamoja na hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali wakati wakitafuta maji.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, amewataka wananchi wa Masuguru kutunza mazingira na vyanzo vya maji ili kuhakikisha mito inaendelea kutiririsha maji na mradi huo unakuwa endelevu.

Sauti ya Mhe.Deogratius Ndejembi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Sauti ya Deogratius Ndejembi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Juma Aweso, ameelezea changamoto mbalimbali ambazo wananchi wa Masuguru na Wilaya ya Nanyumbu kwa ujumla wamekuwa wakikabiliana nazo kutokana na uhaba wa maji, akibainisha kuwa mradi huo wa shilingi bilioni 38 unalenga kuzitatua changamoto hizo na kuboresha maisha ya wananchi.

Sauti ya Juma Aweso waziri wa maji

Akizungumzia umuhimu wa mradi huo, Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Masuguru, Hassani Saidi Litambo, amesema kwa kipindi cha nyuma wananchi wamekuwa wakikumbwa na madhara makubwa kutokana na kushambuliwa na wanyama wakali wakati wakitafuta maji, hali iliyosababisha baadhi yao kupoteza viungo vya miili yao.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto hiyo iliyokuwa ikiwakabili wananchi.

Sauti ya Hassani Saidi Litambo, Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Masuguru

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wameipongeza Serikali kwa kutekeleza mradi huo, wakisema utawapunguzia adha ya kutafuta maji katika maeneo yenye hatari ya kushambuliwa na wanyama wakali, huku wakiahidi kushirikiana na Serikali katika kulinda vyanzo vya maji na miundombinu ya mradi huo.

Sauti za baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Masuguru