Jamii FM
Jamii FM
16 October 2026, 19:59

Na Gregory Millanzi
Wananchi wamehimizwa kuchukua hatua za kuzuia mazalia ya mbu katika mazingira wanayoishi sambamba na kuzingatia unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto wachanga katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya na ustawi wa jamii.
Masuala hayo yamepewa kipaumbele katika kipindi cha ”Dira ya asubuhi” ambapo kimeangazia umuhimu wa usafi wa mazingira katika kukabiliana na magonjwa yanayoenezwa na mbu, hususan malaria, pamoja na faida za unyonyeshaji wa maziwa ya mama katika ukuaji na maendeleo ya mtoto ambapo wananchi wamepatiwa elimu kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia mazalia ya mbu na umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, kutokana na mchango wake katika kuimarisha kinga ya mwili, ukuaji bora na kupunguza hatari ya mtoto kupata baadhi ya magonjwa.
Pamoja na faida za kiafya, elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu manufaa ya unyonyeshaji katika kuimarisha uhusiano wa mama na mtoto, kupunguza gharama za malezi na kuchangia ustawi wa familia.
Kupitia mijadala na ushauri wa kitaalamu, kipindi hicho kinalenga kuhamasisha familia na jamii kwa ujumla kubadili mitazamo na kuzingatia hatua rahisi za kujikinga na magonjwa, huku zikitoa kipaumbele kwa afya ya mama na mtoto.
Kipindi hicho kimeandaliwa na Gregory Millanzi na kuwasilishwa na watangazaji Mwanahamisi Chikambu na Mussa Mtepa, Bonyeza hapa kusikiliza.