Jamii FM
Jamii FM
19 November 2026, 06:58

TAKUKURU Mkoa wa Mtwara imefanikisha kurejeshwa kwa shilingi milioni 149.9 kwa serikali na sekta binafsi katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026 kupitia shughuli za uzuiaji rushwa, huku ikifuatilia utekelezaji wa miradi 47 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 34.06
Na Musa Mtepa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara, imefanikisha kurejeshwa kwa jumla ya shilingi 149,904,340 serikalini na kwa sekta binafsi katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Septemba 2026, kupitia shughuli za uzuiaji na mapambano dhidi ya rushwa.
Hayo yameelezwa leo, Novemba 18, 2026, na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Bi. Mwanakombo Rajabu, wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kati ya fedha hizo, shilingi 63,519,043.50 zimelipwa kwa Chama cha Msingi cha Mshikamano kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu.
Amesema fedha hizo zilitokana na mauzo ya tani 25,038 za ufuta ambazo hazikuingizwa kwenye mfumo wa mnada wa kidijitali, hali iliyosababisha wakulima kukosa malipo ya stahiki zao.
Aidha, Bi. Mwanakombo amesema TAKUKURU imebaini madeni ya shilingi 1,130,000 yaliyotokana na wadaiwa ambao walikuwa wamefunga biashara zao, kubadilisha shughuli za biashara au kufariki dunia.
Katika hatua nyingine, amesema kiasi cha shilingi 16,490,000 kimelipwa kwa Bw. Salumu Chidandwa, mkazi wa Kijiji cha Mtimwiba, Kata ya Mkuti, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, ambaye alikuwa hajalipwa fedha za mauzo ya korosho zake zenye uzito wa kilogramu 8,400.
Amesema mkulima huyo alikuwa amemuuzia Bw. Robert Itatilo korosho hizo, ambaye aliahidi kumlipa siku iliyofuata lakini akashindwa kutekeleza ahadi hiyo kwa kipindi cha miezi miwili, hadi mlalamikaji alipofika TAKUKURU na kupata msaada.

Pamoja na hatua hizo, Bi. Mwanakombo amesema katika kipindi hicho TAKUKURU imefuatilia matumizi ya fedha zenye thamani ya shilingi bilioni 34.06 katika miradi 47 ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta za barabara, afya, ujenzi, elimu, maji na utawala.

Sambamba na hilo, TAKUKURU Mkoa wa Mtwara imewataka wananchi kushirikiana na taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia simu au kufika katika ofisi za TAKUKURU zilizopo katika halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara.